
Na Shomari Binda-Musoma
WANANCHI wa Kata za Busambara na Kiriba zilizopo jombo la Musoma vijijini wamemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia mradi wa maji ya bomba.
Licha ya kumshukuru Rais Samia wamemshukuru pia mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Profess Sospeter Muhongo kwa ufatiliaji wake wa karibu na kufanikisha kufikiwa na maji safi na salama.
Shukurani hizo wamezitoa kwa nyakati tofauti kwenye Kata hizo wakati wa zìara ya Kijiji kwa Kijiji inayofanywa na mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka.
Wananchi wa Kata ya Busambara wamesema wameangaika kwa muda mrefu na sasa wameondokana na shida ya maji.

Wamesema shida ya maji iliwafanya kushindwa kufanya shughuli nyingine za kiuchumi kwa wakati wakitafuta maji
Mmoja wa wananchi hapo aliyejitambulisha kwa jina la Mukama Mgeta amesema Rais Dkt.Samia ana deni kubwa kwao na malipo yake ni kumpa kura za kishindo kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.
” Tunamshukuru sana Rais Dkt.Samia kwa mradi huu wa maji na sasa tunapata maji safi na salama ya bomba hapa kijijini na hatuangaiki tena kutafuta maji.
” Mbunge wetu Profesa Sospeter Muhongo tunamshukuru pia kwa ufatiliaji wake wa karibu na kutufikishia maji”,amesema.
Akiwa Kijiji cha Mwiringo Kata ya Kiriba kwenye ziara yake ya Kijiji kwa Kijiji mkuu wa Wilaya ya Musoma alimueleza mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji kuhakikisha mwezi machi 15 maji yanatoka

Jimbo la Musoma Vijijini lenye vijiji 68 linayo miradi ya usambazaji wa maji ya bomba ndani ya vijiji vyote 68 iliyokamilika na inayoendelea.
Taarifa ya ofisi ya mbunge wa jimbo la Musoma vijijini iliyotolewa leo februari 15 imesema tenki la ujazo wa lita 500,000 limejengwa Kijijini Mwiringo kwa ajili ya usambazaji wa maji ya bomba ndani ya vijiji vyote sita (6) vya Kata hizo mbili.
Taarifa hiyo imesema mkuu huyo wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka anaufutalia mradi huo na mingine ya Jimboni kwa ukaribu sana.
“RUWASA inaendelea kupongezwa kwa kazi nzuri inazozifanya Jimboni mwetu – kila kijiji kupata maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria au/na kuchimbiwa kisima kirefu cha maji – hongereni sana” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
