Home Kitaifa WANANCHI NYATWALI WAMUAHIDI RC MTAMBI MATUMIZI SAHIHI FEDHA ZA FIDIA

WANANCHI NYATWALI WAMUAHIDI RC MTAMBI MATUMIZI SAHIHI FEDHA ZA FIDIA

Na Shomari Binda- Bunda

WANANCHI wa Kata ya Nyatwali wilayani Bunda wamemuahidi mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambj matumizi sahihi ya fedha za fidia kupisha shughuli za uhifadhi.

Ahadi hiyo wameitoa jana septemba 5 kwenye Kata hiyo wakati wakipokea mfano wa hundi ya malipo hayo yanayotolewa na serikali kupitia Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA)

Wamesema fedha watakazolipwa watazielekeza kwenye kupata makazi mapya na kuweka mazingira mazuri ya maisha kwenye maeneo watakayoamia

Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Nzugumi Mayala amesema ushauri wa mkuu wa mkoa wataufanyia kazi baada ya kupata fedha hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amezindua ulipaji fidia kwa wananchi wanaohamishwa kutoka kata ya Nyatwali wilayani Bunda.

Akizindua ulipaji wa fidia hizo katani hapo RC Mtambi amewataka wananchi wanaopata malipo hayo kuondoka katika eneo hilo na kutumia fedha hizo vizuri kwa maslahi ya familia zao.

“Akili zenu zianze kufikiria jinsi mtakavyopata faida kutokana na utalii, wanaume wenzangu msichukue nyumba ndogo baki na uliye naye, tunza watoto mkaanze maisha yaliyo bora.

“Kama familia muweke mikakati ya pamoja namna ya kuzitumia fedha mtakazopokea ili mpate maendeleo.

“Hili ni eneo la mapito ya asili ya wanyama pia eneo hili linaweza kuwa na manufaa makubwa ya kiutalii hapa Bunda hivyo ni vyema mkaliona eneo hili la hifadhi kama eneo lenye fursa za kiutalii ambazo baadaye zitawasaidia kama lilivyo eneo maarufu la Kogatende Serengeti wanapovuka Nyumbu”, amesema

Kanali Mtambi amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za fidia ambapo malipo haya yataambatana na asilimia saba ya ucheleweshwaji wa malipo tokea uthamini ulipofanyika.

Diwani wa Kata ya Nyatwali, Malongo Mashimo baada kudhuhudia uzinduzi wa fidia Nyatwali kama kiongozi amefurahia unzinduzi wa malipo ya fidia kwa wananchi wake.

Naye Mbunge wa jimbo la Bunda Mjini Robert Maboto amesema wananchi wapewe elimu ya kutosha ya namna zoezi la ulipaji fidia litakavyofanyika.

Kiasi cha shilingi bilioni 45.9 kimetengwa na serikali kwa ajili ya kuwalipa wananchi zaidi ya 3,658 wanaohamishwa kutoka eneo lenye ukubwa wa ekari 14,250.

Serikali inatwaa eneo hilo la Nyatwali kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi endelevu wa mfumo wa ikolojia ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na usalama wa wananchi hao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!