Home Kitaifa WANANCHI NANYALA KUTUMIA SHILINGI MILIONI 56.4 ZA FIDIA YA ARDHI KUJENGA MADARASA.

WANANCHI NANYALA KUTUMIA SHILINGI MILIONI 56.4 ZA FIDIA YA ARDHI KUJENGA MADARASA.

Na Moses Ng’wat, Mbozi.

WANANCHI wa kijiji cha Nanyala, Kata ya Nanyala, wilayani Mbozi, wamekubaliana kwa pamoja kutumia fedha kiasi cha shilingi milioni 56.4
zilizolipwa kama fidia ya ardhi yao na mwekezaji kwa ajili ya kujenga madarasa nane mapya katika shule ya msingi kijijini hapo.

Azimio hilo limefikiwa mwishoni mwa wiki hii, katika mkutano wa hadhara wa kijiji hicho ambao pia ulihudhuriwa na Diwani wa kata hiyo, George Musyani na kufanyika katika uwanja wa mpira wa shule ya Msingi Nanyala.

Fedha hizo zimetolewa na mwekezaji wa Kampuni ya Songwe Cement aliyepatiwa ardhi ya kijiji hicho kiasi cha ekari 47 kwa ajili ya mradi wa uchimbaji wa madini ya Chokaa.

Katika mkutano huo uliofunguliwa na Mwenyekiti wa kijiji hicho, Maneno Mwampungamaarufu kama Kizito, iliamuliwa kuwa fedha hizo zitumike katika mradi wa ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba nane vya madarasa, badala ya fedha hizo kugawanywa kwa mtu mmoja mmoja.

Akizungumza katika mkutano huo, Diwani wa kata hiyo, Musyani aliwapongeza wananchi hao kwa uamuzi wao huo kwa kuwa jambo lililoamua lina manufaa makubwa na ya muda mrefu kwa jamii na maendeleo ya kijiji.

“Ardhi hii mliyoitoa kwa mwekezaji ilikuwa ni yenu na hata fedha zitakazoletwa ni zenu, hivyo naomba kama tulivyokubaliana twendeni tukamalizie ujenzi wa vyumba hivi nane vya madarasa” alisema Musyani.

Alisema katika kuhakikisha vyumba hivyo vyumba hivyo vijengwe kwa ubora mkubwa, Halmashauri ya Wilaya imeunga mkono kwa kutoa Bati 216 ili kupunguza gharama.

Musyani alisema kwa mujibu wa muongozo wa serikali gharama ya kumalizia chumba kimoja ni shilingi milioni 12.5, hivyo kiasi hicho cha shilingi milioni 56.4 kitasaidia kwa kiwango kikubwa kukamilisha mradi huo.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Samwel Mwaleya, akizungumza kwa niaba ya wakazi wenzake alisema wananchi kwa pamoja wameunga mkono fedha hizo za fidia kutumika katika ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kuwa kuna tija kubwa kuliko fedha hizo angegaiwa mtu mmoja mmoja.

“Sisi kama wananchi tunaunga mkono na kubariki mawazo ya viongozi wetu juu ya fedha zinazotolewa na mwekezaji kwenda kwenye ujenzi wa madarasa kwani kukamilika kwa madarasa hayo kutabadilisha muonekano wa shule yetu” alisema Mwaleya.

Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mwampunga aliwataka wananchi kuendeleza mshikamano wao katika kupigania maendeleo ya kijiji kwa kuwa muda wa malumbano ya kisiasa umemaliziaka hivyo ni muda wa viongozi wapya waliochaguliwa kutekeleza majukumu yao.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!