Wananchi wa kata na Tarafa ya katunguru wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza wamejitolea kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa kituo cha Polisi kilichoanzishwa kwa nguvu za wananchi.
Hayo yalijiri jana tarehe 07 Mei, 2024 wakati Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Naibu kamishina wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa alipotembelea kukagua Maendeleo ya kituo hicho na kuzungumuza na wananchi wa Kata hiyo.
Akizungumza wakati wa mkutano na wananchi hao, kamanda Mutafungwa amewahamasisha kumalizia ujenzi wa kituo hicho kwa wakati ili kiweze kuhudumia wananchi wa eneo hilo na maeneo jirani.
Aidha, kamanda Mutafungwa amechangia kiasi cha Shilingi milioni moja na kuahidi kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kituo hicho kinakamilika na kuanza kutumika.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Katunguru Sadiki mola amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wananchi katika ujenzi wa kituo hicho.
Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Katunguru Lukas Lushoshaga amesema ili Polisi wafanye kazi kwa uadilifu wanatakiwa kuwa na mazingira bora ya kufanyia kazi hivyo kituo hicho kitakapokamilika kitakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Kata ya Katunguru na Kata za jirani.