Na.Faustine Gimu, Missenyi Kagera.
Wananchi wa Bunazi Wilayani Missenyi Mkoani Kagera wamefurahishwa na hatua mbalimbali za wizara ya Afya na ubunifu wa utoaji wa elimu ya kujikinga na Ebola kwa kutmia ubunifu kama njia ya magari maalum ya matangazo, vipeperushi, kutgawia bure mavazi maalum ya sisi waendesha bodaboda pamoja na kuwatumia wasanii wa jamii husika na wasanii maarufu ambao wanatumia mbinu mbalimbali kutufanya tusikilize Elimu inayotolewa.
Wakizungumza katika zoezi la uhamasishaji jamii utoaji wa Elimu ya Ebola soko la Bunazi wilayani Missenyi Mkoani Kagera baadhi ya wananchi hao wakiwemo waendesha bodaboda ndugu Azan Musa pamoja na Hamad Hussein wamesema hatua hiyo ya wizara kuelimisha jamii itawafikia watu wengi zaidi.
“Sisi Bodaboda na jamii kwa ujumla tunashukuru sana kwa hatua hii kutokana na kazi zetu maana sisi ni wahanga kutokana na kazi zetu, “Ki ukweli sisi ndio tunaofanya biashara huko njia za panya, na biashara yetu ni nini kubeba abiria sasa kama sijuwi kuna Ebora, sijuwi dalili wala namna ya kujikinga si tatizo kubwa hilo”
”Kwa elimu mliotupatia, sasa najua baadhi ya mambo kuhusu Ebola mfano dalili ni pamoja na homa, maumivu ya mwili, kutokwa damu machoni, mdomoni, masikioni na kutapika. Nimeyajua haya haraka haraka kutokana na mnavyotumia picha nyimbo wa kutushawishi kuja hapa kwani nimevutiwa na vionjo mbalimbali ikiwemo wasanii hivyo nami baada ya kupatiwa reflector hii bure kabisa nitakuwa balozi kwa wengine pia “amesema Azan Musa .
“Naishukuru sana Serikali kwa kuja hapa Bunazi kwa ajili ya kutoa elimu ya Ebola na nilikuwa na mishe zangu baada ya kuona kuna mambo ya wasanii ,reflector za bodaboda na vipeperushi nikaamua kuachana kwanza na shughuli zangu nipate kitu hiki adimu na Mungu ni mkubwa sijakaa bure hapa nimetoka na reflector bureee, nimepata burudani bure kwa hiyo nawasihi na wengine wanapoyaona magari haya yaliyoandikwa jikinge tuishinde Ebola wasiyapuuzie”amesema Hamad Hussein.
Akizungumza katika zoezi hilo la utoaji wa elimu ya kujikinga na Ebola soko la Bunazi ,Kaimu Mkurugenzi kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya, Dkt.Ama Kasangala amesema wanatumia fursa ya kuwafuata wananchi mahali walipo ili kuweza kupata uelewa zaidi kuhusu jinsi ya kujikinga na Ebola.
“Bado tunaendelea kutoa na mwitikio ni mzuri “amesema Dkt.Ama.
Hata hivyo, Dkt.Ama ameendelea kusisitiza kuwa Ugonjwa wa Ebola bado haujaingia nchini bali hizo ni hatua za tahadhari mapema katika kuhakikisha ugonjwa wa Ebola hauingii nchini kwani kinga ni bora kuliko tiba.