Home Kitaifa WANANCHI 367 WAHAMA HIFADHI YA NGORONGORO

WANANCHI 367 WAHAMA HIFADHI YA NGORONGORO

Na Mwandishi wetu, Ngorongoro

Muitikio wa wananchi wanaoishi katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuendelea kuhama kwa hiari umepamba moto ambapo leo tarehe 22 Agosti, 2024 jumla ya kaya 79 zenye watu 367 na mifugo 995 zimehama kutoka hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera Handeni na maeneo mengine waliyochagua wenyewe.

Akiwaaga wananchi hao Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii (anayesimamia maliasili) CP Benedict Wakulyamba amesema kuwa kuondoka kwa kundi hilo leo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kulinusuru eneo la hifadhi ya Ngorongoro ambapo wananchi wameendelea kuelimishwa na kuhama kwa hiari kwa ajili ya kuboresha maisha yao na kunufaika na fursa za kiuchumi zilizoko nje ya hifadhi.

“Uamuzi mlioufanya leo mmeonesha na kutambua changamoto mnazokutana nazo ndani ya Hifadhi na kuona ni jambo jema na la busara kuhamia nje ya Hifadhi ili kuweza kuboresha maisha yenu pamoja na kunusuru uhai wa hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni ya kipekee afrika na dunuani kwa ujumla”

CP Wakulyamba amewasisitiza wananchi hao kuwa mabalozi wa kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma za kijamii na fursa za kiuchumi Kijiji cha msomera na kuwafahamisha wenzao waliobaki wajue fursa hizo na kuhamasika kuhama.

Ametoa tahathari kuwa wapo baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakihamia Msomera kinyemela bila kufuata utaratibu uliowekwa na kuleta changamoto kwa ndugu zao wanaowakuta huko na kuwasihi kuwa kufuata utaratibu na miongozo iliyowekwa ili wawe wakazi halali wa maeneo wanayopenda kuhamia.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kuhamisha wananchi wa Ngorongoro kwa hiari, Afisa Uhifadhi mkuu na Meneja mradi wa kuhamisha wananchi kwa hiari PCO Flora Assey amebainisha kuwa tangu zoezi hilo lilipoanza mwezi Juni, 2022 hadi kufikia mwezi agosti, 2024 takriban kaya 1,598 zenye watu 9,618 na mifugo 39,779 imeshahama ndani ya hifadhi kwenda Kijiji cha Msomera na maeneo mengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!