Home Kitaifa WANANCHI 119 KUTOKA ENEO LA HIFADHI YA NGORONGORO WAPOKELEWA NA KUKABIDHIWA MAKAZI...

WANANCHI 119 KUTOKA ENEO LA HIFADHI YA NGORONGORO WAPOKELEWA NA KUKABIDHIWA MAKAZI YAO MSOMERA

Na Mwandishi wetu, Handeni
Tanga.

Jumla ya kaya 26 zenye watu 119 na mifugo 300 zilizokubali kuhama kwa hiari kutoka ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro zimepokelewa rasmi katika Kijiji Msomera, Wilayani Handeni Tanga tarehe 28 Septemba, 2024.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Katibu tarafa wa tarafa ya Sindeni Bw. Baraka Nkatura alisema kwamba Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kuwa wananchi hao waliokubali kuhama kwa hiari wanapatiwa huduma bora kama walivyoahidiwa.

“Leo tumewapokea rasmi, mtakabidhiwa makazi yenu mapya yaliyoandaliwa na Serikali ambako mtapewa nyumba yenye vyumba vitatu iliyojengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa hekari 2.5, kuna maeneo yaliyotengwa mahususi kwa ajili ya shughuli za malisho na kilimo ambayo mtaonyeshwa na wataalamu wetu ndani ya siku chache zijazo” alisema Baraka

Akiongoza zoei la kugawa nyumba Msimamizi msaidizi wa ujenzi wa nyumba Msomera kwa upande wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Faudhi Bossa alieleza kuwa ujenzi wa nyumba 2,500 kwa Kijiji cha Msomera umekamilika na wapo tayari kwa ajili ya kuendelea kupokea wananchi hao.

“Tumepokea kaya 26 ambazo leoleo tunawakabidhi makazi yao ikiwa ni nyumba yenye vyumba vitatu iliyojengwa kwenye eneo la hekari 2.5. nyumba hii ina umeme tayari na tumeweka maji ndoo mbili za kuanzia ili waweze kutumia kwa ajili ya mahitaji yao binafsi” Alisema Bossa

Baada ya kukabidhiwa nyumba akitokea Ngorongoro, Bw. Meleji Laitayok alisema kwa
“Nimefurahi sana nimepata Nyumba nzuri kwani kule Ngorongoro tulikuwa hatuwezi kujenga wala kufanya shughuli za maendeleo, lakini sasa tukiwa huku tunaweza kujiendeleza na kuboresha maisha yetu zaidi”

Kwa upande wake Bw. Daniel Panin kutoka kijiji cha Nainokanoka Ngorongoro ameshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa fursa ya kuboresha maisha yao nje ya hifadhi na kuahidi kuwa watatumia vyema fursa hii kujiendeleza na kuboresha maisha yao.

Serikali inaendelea na ujenzi wa nyumba kijiji cha Msomera kwa ajili ya wananchi wanaohama kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari ambako hadi Septemba 28, 2024 jumla ya nyumba 3003 zimekwisha kamilika kwa awamu mbili za ujenzi na kati ya hizo 1,473 zina watu na zingine zinasubiri wananchi wanaondelea kujiandikisha kuhama kwa hiari

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!