Na. Elimu ya Afya kwa Umma .
Katika jitihada za Serikali za kuhakikisha kila jamii inafikiwa na elimu kuhusu tahadhari na kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Marburg baada ya kuripotiwa Mkoani Kagera, Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ) Kambi ya Kaboya Wilayani Muleba Mkoani Kagera wamevutiwa na hatua zinazofanywa na Wizara ya Afya za uelimishaji kuhusu tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo.
Akizungumza mara baada ya kutembelea kutoa elimu katika kambi ya Jeshi Kaboya Wilayani Muleba Mkoani Kagera, mwakilishi kutoka Wizara ya Afya,Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Beauty Mwambebule amesema Wizara ya Afya, na Wadau wengine wana wajibu wa kuhakikisha kuwa Taasisi zote zinafikiwa na elimu hii ikiwemo Majeshi, ambapo katika kambi hiyo takriban wanajeshi 72 wameweza kupatiwa elimu ya ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Marburg.
“Pamekuwa na hamasa ya juu sana katika eneo hili la jeshi ambapo kikubwa ambacho nimekiona katika kambi la jeshi hili ni ule utayari wa kuomba na familia zao ziweze kufikiwa na elimu ya ugonjwa wa Marburg na sisi kama Wizara ya Afya na Ofisi ya Mganga Mkuu Mkoa wa Kagera tupo tayari “amesema.
Aidha, Beauty ameushukuru uongozi wa Kambi ya Jeshi Kaboya kwa kuahidi kuja na mkakati wa kuhakikisha kila mwanajeshi anakuwa na vitakasa mikono , kuweka maeneo ya kunawa mikono ikiwa ni pamoja na katika ngazi ya familia ambapo pia Wizara ya Afya imetoa ndoo za kunawia katika kambi hiyo.
“Mwitikio wa wanajeshi ni mzuri sana , kwanza wamehakikisha kila Mwanajeshi hapa ana vitakasa mikono ambacho kinatia moyo kuwa Taasisi kama hizi wapo tayari kupambana na magonjwa ya mlipuko na kila kstation point wapo tayari kuweka ndoo yenye maji tiririka na sabuni ya maji kwa ajili ya kunawa ili kukabiliana na ugonjwa huu “amesema.
Awali Mkuu wa Kambi ya Jeshi ya Kaboya Kamanda Luten Kanali Saleh Nia ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuendelea na hatua za uelimishaji kila Taasisi huku akiomba elimu ya ugonjwa wa Marburg itolewe pia katika familia za wanajeshi ndani ya kambi hiyo.
Kwa upande wao baadhi ya Askari wa Jeshi la Wananchi(JWTZ) katika kikosi cha Kaboya akiwemo 2Lt Charles Kakuyu pamoja na 2Lt Irene Aaron Lukyaa wamesema kupitia elimu waliyoipata itawasaidia kujikinga na ugonjwa wa Marburg .
“Kuanzia leo nimejifunza namna ugonjwa huu unavyoweza kuenezwa kupitia wanyamapori ,majimaji mwilini na dalili zake mfano kutokwa na damu, pia nimejifunza kuwa iwapo nitaona kuna mtu ana dalili nina wajibu wa kutoa taarifa mamlaka husika au kupiga simu bure 199”amesema 2Lt Irine Lukyaa”.
MWISHO