Na Scolastica Msewa, Mikumi.
Watanzania zaidi ya elfu 60 wamefika kutembelea hifadhi ya taifa ya mikumi katika kipindi cha mwezi juni 2022 hadi mwezi juni mwaka huu baada ya hamasa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan utalii kupitia sinema ya the Royar tour ambapo kwa mwaka 2023/24 watanzania zaidi ya laki moja wanatarajiwa kutembelea hifadhi hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa habari wakati akiwapokea Wanachama 162 wa kikundi cha kufa na kuzikana cha Mlandizi family cha Kibaha mkoani Pwani walipofika katika Hifadhi ya taifa ya Mikumi iliyopo mkoani Morogoro Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ignace Gara amesema baada ya kutokea ugonjwa wa covid 19 duniani idadi ya watalii ilipungua katika hifadhi hiyo lakini baada ya hamasa ya Rais Dkt. Samia idadi ya watalii imeongezeka.
Amesema alichofanya Rais Dkt. Samia kutangaza na kuhamasisha yeye mwenyewe utalii hajawahi kufanya Rais yeyote barani Afrika hivyo imekuwa ni hamasa kubwa ya utalii ndani na nje ya Tanzania kufika kutalii katika mbuga mbalimbali nchini.
Aidha Kamishna Msaidizi mwandamizi huyo wa Hifadhi ya Mikumi amewapongeza Kikundi cha kufa na kuzikana cha Mlandizi family kwa kutembelea hifadhi hiyo kujionea vivutio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujionea wanyama wapolini katika hifadhi ya Mikumi.
Amewataka watanzania wengine pia waige tabia hiyo na wao wafike kutembelea hifadhi za taifa kwani katika hifadhi hizo kuna vivutio vingi vizuri ambavyo ni burudani ambayo huwezi kuipata sehemu nyingine isipokuwa mbugani.
Mwenyekiti wa kikundi cha Mlandizi Family Eli Achahofu Paulo amesema kikundi chao kina wanachama kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania bara na visiwani ambao husaidiana masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja katika misiba lakini awamu hii wameamua kufika mbugani hapo ili kujionea kazi kubwa inayofanywa na Rais Dkt. Samia katika upande wa utalii nchini.
Aidha amewaomba na watanzania wengine pia kutembelea hifadhi za wanyama nchini ilikuungana na Rais katika jitihada zake za kuhimiza utalii wa ndani nchini.
Naye Msemaji wa kikundi cha Mlandizi family Nyabhise Wandwi ameishauri serikali kuanzaisha utaratibu wa wanafunzi kuanzia shule za msingi za serikali kutembelea kwenye hifadhi za wanyama kujionea na kujifunza mengi kupitia utalii huo wa wanyama poli nchini.