WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa kote nchini wahakikishe kunakuwa na idadi ya kutosha ya mawakala wa pembejeo za kilimo katika maeneo yao ili zoezi la kufikisha mbolea kwa wakulima litekelezeke kwa ufanisi.
Amesema hayo leo (Desemba 14, 2022) alipozungumza na wakazi wa Kata ya Majimoto, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi ambako yupo kwenye ziara ya kikazi. Amewataka viongozi hao wawasimamie mawakala hao watekeleze zoezi hilo ipasavyo.
Aidha Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha shilingi bilioni 150 kama ruzuku ya ununuzi wa mbolea “Nataka niwaambie mawakala. Fedha ya ruzuku kutoka Serikalini kwa ajili ya malipo yenu ipo, pelekeni pembejeo kwa wakulima, muhimu mfanye biashara kwa weledi na uaminifu mkubwa.”
Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa Mkoa wa Katavi ambao una mawakala 10 wa kuuza pembejeo kwa wakulima umetengewa tani 4,956 za mbolea ambapo tayari tani 3,977 zimeshafikishwa mkoani humo.
Kadhalika Waziri Mkuu amewataka wakulima kuendelea kujihusisha na shughuli za kilimo hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha kwa kuwa mbolea ipo na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia amesisitiza Mkoa wa Katavi upate mbolea ya kutosha.