Home Kitaifa WAKULIMA 227,905 WA KAHAWA WAKABIDHIWA MICHE YA BURE

WAKULIMA 227,905 WA KAHAWA WAKABIDHIWA MICHE YA BURE

Na Gideon Boniface, Lushoto

WAKULIMA wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wamegawiwa bure miche ya kahawa 227,905 ikiwa ni jitihada za kuweza kurejesha tena zao hilo ambalo lilishamiri zaidi ya miaka 50 iliyopita kwenye wilaya hiyo.

Jitihada za kurejesha zao hilo linafanywa na Bodi ya Kahawa Tanzania, Kanda ya Kaskazini ili kuwawezesha wataalamu wa kilimo kwenye halmashauri ikiwa ni pamoja na kugawa miche na kutoa mafunzo kwa maofisa ugani na wakulima.

Uzinduzi wa kugawa mbegu hizo umefanyika mwishoni mwa wiki huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro ambaye alizungumza na wakulima hao waliotoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kushiriki zoezi la kugawa miche kwa wakulima, Lazaro alisema zao la kahawa ni moja ya mazao ya kimkakati kwenye wilaya hiyo, hivyo wanataka kurudisha kilimo hicho kama ilivyokuwazaidi ya miaka 50 iliyopita.

Kazi yetu viongozi wa Wilaya ya Lushoto ni kuona wakulima wetu wanakuwa na mazao ya kimkakati hasa ukichukulia Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka nguvu nyingi kwenye kilimo. Na mwaka jana Bodi ya Kahawa Tanzania, Kanda ya Kaskazini iligawa miche 68,000 kwa wakulima wetu, lakini tukaona hiyo haitoshi, ni vizuri Lushoto ikawa na kitalu cha miche, na tumepanda miche 300,000, na leo hii wakulima wanagawiwa miche 227,905.

Tunataka kuliendeleza zao la kahawa kama ilivyokuwa siku za nyuma, na zao hili ni la kimkakati. Wilaya ya Lushoto ina mazao ya kimkakati matano ambayo ni kahawa, mkonge kule chini eneo la tambarare, parachichi, ngano na chai kule Bumbuli. Kwa mazao hayo, wakulima wetu watakuwa na uhakika wa kipato” alisema Lazaro.

Naye Afisa Maendeleo wa Kahawa Kanda ya Kaskazini Saidi Ng’ombo alisema, Bodi ya Kahawa Tanzania imeweka malengo ya kufikisha uzalishaji wa tani 300,000 za kahawa safi ifikapo mwaka 2025, hivyo katika kufika lengo hilo katika msimu wa 2022/23, iliweka lengo la kuzalisha miche 2,000,000 katika Kanda ya Kaskazini na kuigawa kwa wakulima wa kanda hiyo.

“Katika kutekekeleza azma hii na ikiwa Lushoto ni miongoni mwa wilaya zinazozalisha kahawa kwa kiwango cha chini, na kwa kuzingatia mapendekezo ya Mbunge wa Mlalo Rashid Shangazi, bodi imeanzisha kitalu cha miche ya kahawa kilichopo maeneo ya Jegestali, Lushoto mjini chenye uwezo wa kuzalisha miche 300,000. Hata hivyo, bodi mpaka sasa imeshazalisha miche 227,905 ambayo iko tayari kwenda shambani kipindi hiki cha masika.

Aidha, miche hii inatarajia kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 50 hadi 75 kwa mwaka kwa msimu wa 2020/21 2021/22, ambapo kwa misimu ya nyuma wilaya hii ilikua ikizalisha tani 250 kwa mwaka, na kufika hadi tani 500 kwa mwaka ifikapo 2025/26, ambapo itachangia kuongeza kwa ukuaji wa uchumi kwa wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na Halmashauri ya Bumbuli, na hata kuongeza mapato kwa halmashauri hizi” alisema Ng’ombo.

Kaimu Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto George Medeye alisema miche 227,905 iliyogawiwa ina uwezo wa kupandwa kwenye eneo la ekari 228. Na kuongeza kuwa uwezeshwaji wote unaofanyika kwa ajili ya kuinua tena kilimo cha kahawa wilayani humo, unafanywa na Bodi ya Kahawa Tanzania, Kanda ya Kaskazini.

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!