
Kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, amewataka wakazi wa Wilaya ya Tarime, Mara, kuripoti kwa Mamlaka husika watoa huduma ndogo za fedha wasiosajiliwa au wanaotoa huduma kinyume cha sheria.
Ameyasema hayo Machi 17,2025 wakati wa utoaji wa elimu ya fedha katika maeneo ya Manga, Sirari, Matombo, Nyamwaga, Ganyange na Gorong’a.

Bw. Kimaro amesema kuwa watoa huduma wasiofuata sheria wanachangia kudhoofisha maendeleo ya wananchi, jambo ambalo Serikali haiwezi kulifumbia macho. Ameeleza kuwa utoaji wa elimu ya fedha unalenga kuwawezesha wananchi kutambua haki zao, kuelewa huduma sahihi za fedha, na kuripoti changamoto kwa mamlaka husika.
Aidha, amewashauri wananchi kusimamia matumizi ya fedha zao kwa uangalifu na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima kama sherehe na ngoma zisizo na tija. Badala yake, amewahimiza kuwekeza kwenye mifuko ya uwekezaji wa pamoja na hati fungani za Serikali ili kujihakikishia maendeleo ya kifedha.

Aidha Kwa mujibu wa Utafiti wa FinScope wa mwaka 2023, ni asilimia 53.5 pekee ya nguvukazi nchini wanaotumia huduma rasmi za fedha, hali inayowaacha Watanzania wengi bila fursa za kuboresha maisha yao. Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya huduma rasmi za fedha ili kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika sekta hiyo.
Programu ya Elimu ya Fedha kwa Umma iliyoanza Mei 2024, tayari imefikia mikoa 15, huku Mkoa wa Mwanza ukiwa eneo linalofuata. Bw. Kimaro amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo kwa manufaa ya maisha yao ya kifedha.