Na Scolastica Msewa, Kibaha
Wakala wa Vipimo Tanzania WMA wametoa wito kwa Watanzania wenye mashaka na kipimo chochote wanachopimiwa katika kupata huduma au mahitaji mbalimbali ili kikahakikiwe na Wakala wa Vipimo kwaajili ya kujiridhisha na kipimo anachopimiwa kama ujazo, urefu au uzito kulingana na thamani ya fedha wanayolipa inaendana na bidhaa au huduma wanayopata.
Hayo yamesemwa Misugusugu Kibaha mkoani Pwani na Meneja wa sehemu ya viwango na uhakiki wa Vipimo katika Wakala wa Vipimo Tanzania WMA Magesa Biyani wakati wa zoezi la uhakika wa Vipimo vinavyotumika kuhakiki Vipimo vya kupimia bidhaa na kutolea huduma kwa wananchi, viwandani sehemu mbalimbali nchini.
Amesema Wakala wa Vipimo Tanzania WMA hufanyia uhakiki wa vifaa na vitendeakazi vyao vya uhakiki wa huduma na bidhaa mara moja kwa mwaka ilikuhakikisha uhakiki wao unafanyika katika usahihi unaotakiwa kitaifa na Kimataifa.
Amesema zoezi hilo linahusisha uhakiki wa Vipimo vinavyotumika kuhakiki ujazo, urefu, uzito na Vipimo vingine vyote vinavyohusika katika ukaguzi katika Nchi yetu ambapo ni zoezi linalohusisha uhakiki wa Vipimo vya kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani.
“Timu yote ya kutoka Tanzania nzima Bara na Zanzibar wapo hapa kuweza kuhakikisha kwamba vitendea kazi vinavyohusika katika uhakiki wa Vipimo nchini vinahakikiwa hapa”
“Kama mnavyojua kwamba Vipimo vinasaidia nchi yetu kwasababu tunapokuwa na Vipimo sahihi hata biashara zinaenda vizuri na kwa usahihi kwani kila mtu anapata kile kinachostahili kulingana na thamani ya fedha anayolipa”
“Vile vile zoezi hili linazuia udanganyifu unaofanyika wakati ambapo muuzaji anahitaji kupata faida kuliko kile ambacho anampatia mteja wake hasa kipindi hiki tunapoelekea sikukuu watu hufanya udanganyifu lakini niwahakikishie tu wananchi kwamba Vipimo vyetu ni sahihi na tunavihakiki hapa ili viweze kuwa sahihi”
“Yaani hata inapokuja masuala ya bucha, madukani Vipimo vyetu vipo sahihi lakini kama kutakuwa na changamoto unaona kwamba umepunjwa tafadhali tuwasiliane kwa namba ya mawasiliano kwa Tanzania nzima 0800110097 mkoa wowote tutakuja haraka kukusaidia ili uweze kupata thamani ya fedha uliyolipa” alisema Magesa.
“Wakala wa Vipimo Tanzania WMA tunafanya kazi yetu vizuri ilikuhakikisha kila mwananchi anafanya biashara yake vizuri na kwa usahihi ndani ya nchi na nje ya nchi kwani Vipimo vyote duniani huakikiwa ilikuhakikisha kwamba vipo sahihi kati ya nchi na nchi pia”
+++++++++