Home Afya WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII 1322 WAJENGEWA UWEZO KUKABILIANA NA MARBURG

WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII 1322 WAJENGEWA UWEZO KUKABILIANA NA MARBURG

Katika kukabiliana na Ugonjwa wa Marburg ulioripotiwa rasmi mnamo tarehe 21 Machi, 2023 mkoani Kagera, Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara zingine za Kisekta pamoja na Wadau mbalimbali inaendelea kutekeleza mikakati ya uelimishaji na uhamasishaji jamii ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo  Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii  1,322 katika Mitaa, Vijiji na Vitongoji vyote vya Halmashauri ya Bukoba Vijijini na Manispaa ya Bukoba. 

Hayo yamebainishwa leo April 8, 2023 katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera na  Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma ,Wizara ya Afya Dkt. Tumaini Haonga wakati  akizungumza katika mwendelezo wa utoaji wa elimu  ya afya kuhusu kinga na tahadhari dhidi ya Ugonjwa huo.

Kupitia Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Serikali imetekeleza mikakati mbalimbali ili kuzuia ugonjwa huu usienee maeneo mengine nchini. Ili kuwafikia wananchi  mahali ambapo wanapatikana, Serikali inawatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kwa kuwajengea uwezo wahudumu wapatao 1322 ambapo kati yao Wahudumu wanatoka Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba na Wahudumu wanaobaki wanatoka katika Halmashauri ya Bukoba Vijijini” amesema.

Dkt. Haonga amesema sambamba na kuwatumia Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii katika kutoa elimu ya afya katika maeneo mbalimbali, Serikali pia imetoa magari 8 maalum ya matangazo kwa ajili ya utoaji wa elimu ya Ugonjwa wa Marburg katika maeneo mbalimbali hususan sehemu zenye mikusanyiko.

Utoaji wa magari haya 8 ni kuweka wigo mpana zaidi wa kuelimisha na kuhamasisha wananchi kupata uelewa na kuzingatia njia za tahadhari dhidi ya ugonjwa huu”amesema Dkt. Haonga.

 Dkt. Haonga ameendelea kufafanua kuwa katika kuendelea kuelimisha jamii, makundi muhimu wakiwemo viongozi wa dini wamepewa kipaumbele katika suala la uelimishaji ambapo hadi kufikia Aprili 6, 2023 takribani viongozi wa dini  310 walijengewa uwezo mkoani Kagera kutoka Taasisi mbalimbali za Dini .

Kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), Shirika la Tanzania Interfaith Partneship (TIP) na Uongozi wa Mkoa  tumeweza kuwafikia viongozi wa dini 310 kwa ajili ya kuwajengea uwezo sambamba na hilo tunaendelea kutoa vielelezo vya elimu kuhusu ugonjwa wa Marburg” amesema.

 Katika uelimishaji kwa Taasisi za Umma Dkt. Haonga karibu shule zote zimeweza kufikiwa pamoja Taasisi zingine ikiwemo magereza, sehemu za Ulinzi na Usalama ikiwemo jeshini na vielelezo vyote vya kutolea elimu vimekuwa vikitolewa kwenye taasisi hizo ambapo Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Tanzania Red Cross Society) kimekuwa kikishirikiana na Wizara ya Afya katika utoaji wa elimu ya afya kwa umma.

Kwa upande wake Mganga Mkuu Mkoa wa Kagera Dkt. Issessanda  Kaniki amesema baada ya kuunganisha nguvu kwa Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Majanga, Wizara ya Maendeleo ya Jamii pamoja na Wadau pamekuwa na matokeo chanya katika suala la uelimishaji.

Baada ya kuunganisha nguvu kupitia Wizara yetu ya Afya ,Wizara zingine za Kisekta pamoja na wadau mbalimbali mwitikio ni mkubwa ,watoa huduma ngazi ya jamii kwa kushirikiana na Tanzania Red Cross Society (TRCS) wameendelea kufikia jamii katika maeneo tofauti, hivyo nitumie nafasi hii kuwaomba wananchi wa Kagera waendelee kutoa ushirikiano kwa kuzingatia njiq za kinga na tahadhari zinazoshauriwa kitaalamu”amesema.

Naye Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji, Thomas Fussy amesema wataendelea kushirikiana na jitihada zinazofanywa na Wizara ya Afya za kuhakikisha wageni wote wanaowahudumia wanazingatia kanuni za afya  ikiwemo kuhamasisha wananchi kunawa mikono mara kwa mara.

Mkoa wa Kagera una mipaka saba, kupitia elimu tuliyopewa na Wizara ya Afya kupitia Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, tutaisambaza katika sehemu mbalimbali tunazotoa huduma ikiwa ni pamoja na sehemu za mipakani hivyo tunaipongeza sana Wizara ya Afya kwa kujidhatiti katika kutoa elimu kila mahali “amesema.

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!