Na Magreth Mbinga
Serikali na wadau hususani vijana wameombwa kuhakikisha kuwa wazee wanapata haki zao stahiki pamoja na kuimarishwa kwa sheria na kuondolewa kwa mifumo kandamizi kwa wazee kwani kadri siku zinavyokwenda wazee wanaongezeka na vijana nao wanaelekea uzeeni.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Balozi Gertrude Mongella katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya kuchangia ujenzi wa kituo cha kuhudumia wazee cha Kasulu Mkoani Kigoma ambacho kitasaidia kutoa huduma mbalimbali kwa wazee ikiwemo hospitali, makazi na sehemu ya mazoezi na burudani.
” kituo hiko kitakuwa ni sehemu ya kutoa uelewa zaidi kwa wazee, maarifa na mfumo wezeshi kwa wazee kupata elimu zaidi kulingana na kuendelea kukua kwa teknolojia na kuwaepusha na kejeli za watu kuwaona wamepitwa na wakati”amesema Mongela.
Pia Mkurugenzi Mtendaji Endeleza Wazee Kigoma na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wazee Tanzania Mama Clotilda Kokupima amesema ujenzi was kituo cha kutunza wazee umeanza muda kidogo baada ya kupata eneo lenye ukubwa wa hekali tano Mkoani Kigoma nia ni kujenga majengo kwaajili ya starehe na matunzo ya wazee kwa kupunguza upweke na msongo wa mawazo pamoja na kupata matunzo mbalimbali.
“Itakuwepo sehemu ya mazoezi ya viungo ,sehemu ya kuendeleza vipaji kwa wale ambao walikuwa wafanya kazi pia kutakuwa na hospitality ambayo itasaidia wazee kutibiwa kwa urahisi sambamba na sehemu ya kupumzika na kuweza kuzungumza mambo yao na sehemu ya kufundisha viongozi was mabaraza ya wazee ” amesema Mama Kokupima.
Aidha Mama Kokupima amesema wazee watapata chakula kizuri kilichopikwa kwa lishe maana wazee waliowengi wanakosa chakula na wengine wanapata kisichokuwa na lishe lakini watakao baatika kufika pale watakuwa wanapimwa afya na kupata lishe bora ili kuongeza afya yao kwa namna moja au nyingine.
Sanjari na hayo Mratibu wa ujenzi wa kituo cha mfano cha malezi ya wazee Carolyn Kandusi amesema lengo kubwa la uzinduzi wa uchangiaji huo ni kuanza safari ya kuwakaribisha Watanzania wenye mapenzi mema kuanza kufikiria swala zima la uzee sababu miaka hamaini ijayo Tanzania ambao ni vijana wa sasa wataongeza idadi ya wazee.
“Kuwepo hapa Leo katika uzinduzi wa kujenga kituo hiko cha mfano ni katika mwanzo wa kuanza kuangalia katika Sera na uhalisia tunajiandaaje katika ongezeko la wazee ambao wataongezeka na wito wangu kwa Watanzania ni kuungana na Endeleza Wazee Kigoma kwa hali na mali ili kuweza kufikia malengo ambayo wameweka ya kujenga kituo hiko cha mfano” amesema Kandusi.
Vilevile Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoani Lindi Abdallah Mohammed Majumba amesema kituo hiko sio cha Kasulu tu ni kituo ambacho wazee kutoka sehemu yeyote wanaweza kufika hapo kupata huduma na vijana wajali kwamba wazee wao wanahitaji matunzo sababu na wao wanaenda hukohuko.