Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania FEMATA John Bina amewataka wachimbaji wadogo nchini kuacha kuilalamikia Serikali’ badala yake waishauri kuhusu wanachokitaka kwa maslahi ya taifa.
Amesema hayo wakati afungua kongamano la siku ya pili ya Maadhimisho ya Wiki ya Madini mwaka 2024 kwa wachimbaji wadogo nchini lililofanyika katika ukumbi mdogo wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Amesema kupitia makongamano ya wiki ya Madini mwaka 2024 wayatumie kuishauri serikali mambo mbalimbali ambayo ni changamoto za wachimbaji Madini wadogo ili serikali itafutie majibu.
“Ndio maana sisi kama Shirikisho tunaandaa makongamano na mikutano maana yake ni kuishauri Serikali na Viongozi kwasababu sisi ndio wenye sekta kwani huwezi kuwa mwanachana wa FEMATA kama sio mchimbaji wa madini ili uwe na uchungu na kile unachozungimzia” alisema Bina.
Mkuu wa idara ya biashara wa Bank ya NMB Alex Mgeni amewataka Wachimbaji wadogo wa Madini kujikita katika kuchimba Madini mkakati ambayo Soko lake ni kubwa kitaifa na Kimataifa.
Alisema madini hayo ya kimkakati hutumika sana katika shughuli za kiteknolojia katika utengenezaji wa ikiwemo betri za magari, maji ya betri, vifaa vya simu hivyo wawekeze kwenye Madini hayo ili waweze kunufaika na uchimbaji wao wa madini hayo.
“Pia wasije kubaki nyuma katika uchimbaji huo wa madini ya kimkakati na wakawaachia Wachimbaji wageni kutoka nje wakanufaika maana yake hata mapato mengi hayatabaki Tanzania yataenda nje ya nchi” alisema Alex.
Mwenyekiti wa wauzaji na wanunuzi wa Madini nchini -TAMIDA – Othuman Tharia amesema wanakamilisha viwanda viwili vya kuongezea thamani ya Madini yenye thamani ilikuhakikishia uhakika wa Soko la Madini wanayochimba nchini.
Alisema viwanda hivyo anajenga wilayani Kahama mkoani Shinyanga na Katika kisiwa cha Zanzibar ambako watapata kuuza na kununua madini hayo ya yenye thamani katika bei elekezi ya serikali.
Naye Mwenyekiti wa wachimbaji wa Wadogo mkoa wa Ruvuma Kasimu Pazi amemtaka Waziri wa Madini nchini Antony Mavunde atekeleze agizo la Dkt Philip Mpango la kuto kumnyang’anya mchimbaji mdogo kumposha mchimbaji mkubwa kwa kisingizio cha eneo hilo lilikuwa la wachimbaji wakubwa.