Katibu wa Wabunge vinara wa Ustawi wa Jamii Mhe.Justine Nyamoga amesema wapo tayari kushirikiana na Serikali kukemea vitendo vya ukatili kwenye jamii.Mhe. Nyamoga ameyasema hayo Jijini Dodoma Juni 21, 2022 katika kikao kazi cha kuwajengea uwezo wabunge vinara wa Ustawi wa Jamii kuhusu utekelezaji, uendeshaji na usimamizi wa Afya mbalimbali za Ustawi wa Jamii katika ngazi ya Halmashauri.
“Sisi wabunge vinara tunawajibu wa kuwa mfano kwa Jinsi ambavyo tunaenenda Kwa kukataa vitendo vya ukatili na kupaza sauti kuhusu vitendo hivyo popote tutakapokuwa iwe ndani au nje ya Bunge katika kuiunga mkono Serikali yetu” amesema Nyamoga.
Nyamoga amepongeza pia hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Wizara inayohusika na Masuala ya Ustawi wa Jamii pamoja na kuridhia katika ajira zinazotarajiwa kuwepo na Maafisa Ustawi wa Jamii ambapo amesema itasaidia kuondoa mkanganyiko uliokuwepo na kuimarisha utendaji
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akifungua kikao hicho, amewapongeza wabunge Kwa hatua ya makusudi kuamua kuunda kikundi cha vinara kwa ajili ya kusaidia Jamii katika suala la ukatili wa kijinsia kuhakikisha unakwisha.
Mhe. Mwanaidi amewaomba wabunge hao kutoa elimu kuhusu ukatili wowote na madhara yake na kuwaeilimisha wananchi kushiriki katika kutoa ushahidi mahakamani kwa wanaokabiliwa na vitendo hivyo.
Ameongeza kwamba bado kuna upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri hali inayochangia utoaji wa Huduma za Ustawi kutopatikana kwa urahisi.
“Huduma za Ustawi wa Jamii zinahitaji kufikia Jamii na Makundi yenye mahitaji Maalum kwa wakati ili kutatua changamoto zinazowakabili ili washiriki kikamilifu katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa, hata hivyo kuna idadi ndogo ya Maafisa Ustawi wa Jamii wanaopaswa kusaidia na kutoa huduma hizo” amesema Mhe. Mwanaidi.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Afya, lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe amewashukuru wabunge vinara kwa kuisaidia Serikali kusukuma mbele masuala ya Ustawi wa jamii tangu kikundi cha wabunge hao vinara kianzishwe mwaka 2021.