Home Afya WAAJIRI WATAKIWA KUTAMBUA HAKI YA WAFANYAKAZI KUNYONYESHA WAKIWA KAZINI NA KUWATENGEA ENEO...

WAAJIRI WATAKIWA KUTAMBUA HAKI YA WAFANYAKAZI KUNYONYESHA WAKIWA KAZINI NA KUWATENGEA ENEO MAALUMU

Na Magrethy Katengu

WAAJIRI wa wafanyakazi katika sekta rasmi na zisizo rasmi wamesisitizwa kuwatambua wakina mama wanaonyonyesha watoto kwa kuwatengea sehemu maalum na kuwapatia muda wa angalau dakika kadhaa ili kusaidia wawapo kazini ili waendelee kuwapatia watoto stahiki yao ya kunyonya kwani kufanya hivyo ni kuleta ukuaji mzuri wa watoto kiakili,na kuwa na afya njema.

Naibu waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa wiki ya unyonyeshaji inayoadhimishwa kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 8 kwenye ukumbi wa ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam pia amebainisha kuwa miongoni mwa changamoto zinazokabili watoto kukumbwa ba magonjwa,ukuaji wa kudhoofu miongoni mwa sababu ni kukosa kunyonya maziwa ya mama kwa wakati na hali hii husababishwa na uelewa duni wa baadhi ya waajiri ,wafanyakazi na jamii kuhusu jambo hilo.

Changamoto zingine ni ukiukwaji wa haki ya uzazi za wanawake wanaofanya kazi katika baadhi ya sekta rasmi na sekta zisizo rasmi ambayo inatokana na kukosekana kwa mazingira wezeshi katika mifumo ya kijamii ya kuwasaidia wanawake waweze kuwanyonyesha watoto wao ipasavyo”

Dkt. Mollel amesema kuwa, mama mjamzito anahitaji matunzo kwaajili ya lishe ya mtoto katika siku 1000 Yaani tangu kutungwa kwa mimba hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka miwili kwani ndio msingi bora wa ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili.

“Katika siku hizi 1000 madhara ya lishe duni hasa udumavu yanaathiri sana maendeleo ya rasilimali watu ya nchi, hivyo ni muhimu mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo na kuendelea kunyonyeshwa huku akipatiwa chakula cha nyongeza hadi anapotimiza miaka miwili au zaidi.” Amesema Dkt. Mollel

Aidha, Dkt. Mollel amesema, watoto wadogo na watu wazima wanapaswa kula lishe bora ili kuwaepusha na magonjwa yanayotokana na kutokula lishe isiyokamilika.

“Kuna magonjwa mengi yanayotokana na kutokula lishe kamili ni vyema watoto na watu wazima kuzingatia hilo, pia lishe inayozidi inasababisha uzito uliozidi na hivyo kusababisha magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Figo na moyo.” Amesisitiza Dkt.Molel

Takwimu zinaonesha kuwa idadai ya watoto wanaonyonyesha maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita imeongezeka kutoka asilimia 58 mwaka 2018 hadi asilimia 64 mwaka 2022.

Pia takwimu za watoto wanaonyonyeshwa ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa imeongezeka kutoka asilimia 53.5 mwaka 2018 hadi asilimia 70 mwaka 2022.

Naye Mwakilishi wa wadau wa Lishe nchini kutoka UNICEF Bw. Patrick Codjia ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa dhamira ya dhati ya kuboresha lishe, afya na maisha ya wananchi wake ikiwa ni pamoja na watoto.

Wakati huo huo Mwakilishi kutoka Shirika la Kimatifa la Kazi(ILO) Bi. Chiku Semfuko ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kutoa muda kwa wanawake kwenda kunyonyesha pia kutenga vyumba maalumu vya kunyonyesha ili kuwapa nafasi wanaonyonyesha.

Aisha wito umetolewa kwa wajawazito nchini kukaa katika mazingira yasiyowaletea msongo wa mawazo katika kipindi chote cha ujauzito na unyonyeshaji ili kufanya maziwa yatoke vizuri na mtoto kupata lishe bora na kukua vizuri kiakili na kimwili akiwa na afya njema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!