Home Kitaifa VIJANA WA FAMILIA MOJA WAFARIKI BAADA YA KUFUNIKWA NA MAWE MKOANI NJOMBE

VIJANA WA FAMILIA MOJA WAFARIKI BAADA YA KUFUNIKWA NA MAWE MKOANI NJOMBE

Watu wawili wa familia moja Okoka Mkaleja (24) na Yusuph Mkaleja (21) wakazi wa halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe wamefariki dunia baada ya kufunikwa na mawe ya mwamba wakati wakichimba madini aina ya Ulanga yanayoelezwa yanapatikana katika kijiji cha Ulanga kata ya Igwachanya wilayani Wanging’ombe.

Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe Claudia Kitta amethibitisha kwa njia ya simu kutokea kwa tukio hilo lililopelekea vifo vya ndugu wawili majira ya saa tano asubuhi Agosti 21.

“Kuna machimbo madogo ya ulanga kwa hiyo ndio walikuwa wanachimba huko na bahati mbaya mawe yakawaporomokea,machimbo haya ni mapya lakini madini yaligunduliwa muda mrefu ndio maana hata kijiji kinaitwa Ulanga lakini yalikuwa hayajachimbwa mpaka hivvi karibuni kampuni moja ya kutoka Makambako ndio walianza kuchimba”amesema DC Kitta

DC Kitta amesema wakati watoto hao wakifukiwa na mawe baba yao ameweza kushuhudia kwa kuwa alikuwepo eneo la tukio na zimepita siku tatu tangu alipofika kwenye machimbo hayo baada ya kuitwa na watoto ili naye aweze kutafuta fedha huku pia akieleza kuwa miili ya vijana hao imehifadhiwa katika hospital ya Ikelu jirani na mji wa Makambako ili kurahisisha taratibu za mazishi “Kwa hiyo baba yao ameshuhudia watoto wake wawili wakifariki”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe,Mahamoud Banga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lilitokea kwenye mgodi uliopo wilayani Wanging’ombe lililopelekea vifo vya vijana wawili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!