Na Shomari Binda-Musoma
VIJANA wanaoshiriki mashindano ya Polisi Jamii Cup Wilaya ya Musoma wametakiwa kutumia mashindano hayo kuzuia uhalifu.
Kupitia mashindano hayo wamekuwa wskipewa elimu kupitia askari Kata juu ya kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu pamoja na kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.
Akizungumza na wachezaji wa timu za Makoko na Mshikamano kwenye uwanja wa Mara sekondari Mkuu wa Polisi Wilaya ya Musoma Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Edison Mwamafupa amesema mashindano hayo licha ya kuinua vipaji vyao watumie elimu wanayoipata kuzuia uhalifu.
Amesema uhalifu haukubaliki na lazima kupambana nao kuhakikisha kwenye jamii unakomeshwa na kuishi kwa usalama.
Mwamafupa amesema wahalifu wanaishi kwenye jamii na wakitolewa taarifa watashindwa kutimiza lengo la uhalifu wao.
” Tutumie elimu tunayoipata kupitia mashindano haya ya Polisi jamii cup kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.
” Wahalifu tunaishi nao kwenye jamii zetu tuwe tayari kuwatolea taarifa kwani kila mmoja akishiriki kufanya hivyo uhalifu na wahalifu utakomeshwa”,amesema
Akizungumzia matumizi ya madawa ya kulevya mkuu huyo wa polisi Wilaya ya Musoma amesema ni kichocheo cha kutenda uhalifu na kuwataka vijana kuachana na matumizi yake.
Katika mchezo uliochezwa leo timu ya Makoko imeondolewa kwenye mashindano hayo na timu ya Mshikamano kwa changmoto ya mikwaju ya penati 5-4
Jumla ya timu 20 zinashiriki mashindano hayo zinazocheza kwa mtindo wa mtoano ambapo kesho kutakuwa na mchezo kati ya Kigera na Kwangwa