Na Magrethy Katengu
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana,Ajira,na Watu wenye Ulemavu Profesa Jamal Katundu amewataka Watanzania wanaopata fursa za ajira nje ya nchi kuhakikisha wanafuata utaratibu mzuri na wanafanya kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa huku wakiwa ili kusaidia Taifa la Tanzania kuheshimika.
Prof. Katundu amesema hayo jijini Dar es salaam wakati wa kuwaaga vijana wapatao 900 ambao wamepata fursa ya ajira nchini Saudi Arabia kwanye kampuni ya ALMARIA inayojihusisha na uzalishaji wa Maziwa, ambapo vijana hao wanatarajiwa kuondoka 50 kuanzia Novemba 9 mwaka huu.
Hata hivyo amesema kuwa vijana hao wanaokwenda kufanya kazi nchini Saud Arabia ni sehemu ya Vijana 408 ambao wamefanyiwa usaili kupitia kampuni ya Bravojob Centre iliyopo hapa nchini kwa kushirikiana na Wakala wa Ajira Nchini(TAeSA ) hivyo kila baada ya wiki moja vijana 50 watapelekwa kufanya kazi katika nchi wanazopaswa kwenda hadi itakapotimia idadi ya 408.
“Ikumbukwe kuwa Serikali ilisitisha Ajira za nje ya nchi baada ya kubaini kuwepo na ajira zisizo na staha,muongozo wa ajira za nje ya nchi ukatangazwa tena Desemba 31 2021 ambapo umezingatia mambo muhimu ikiwemo suala la Ajira zenye staha kama vile kuwepo kwa mikataba ya ajira ,hivyo vijana wote mnaopata fursa za ajira nje ya nchi mtalipwa mishahara na haki zingine kwa mujibu wa sheria”alisema Prof. Katundu.
Prof Katundu amesema kuwa suala la kuwatafutia ajira Watanzania nje ya nchi lipo katika mpango mkakati wa nchi ,ambapo hadi kufikia mwaka 2025 serikali inampango wa kupata ajira milioni nane, hivyo ili kufikia malengo hayo serikali imesajili wakala wa ajira 32 , na serikali kwa sasa ipo kwenye mazungumzo na nchi zipatazo saba ili kuweza kupata fursa za ajira kwa vijana wa kitanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Hemed Mgaza amesema kuwa serikali imetambua umuhimu wa ajira kwa wananchi wake ndio maana imeruhusu watanzania kwenda kufanya kazi na imewasihi kuzingatia nidhamu na tamaduni za nchi husika.
Nae Mkurugenzi wa Kampuni ya Bravojob Centre ,Mbunge Mstaafu Abass Mtemvu amesema kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na serikali kuweza kuwapatia Watanzania ajira nje ya nchi kwani Tanzania inakabiliwa na tatizo la uhaba wa ajira hivyo watanzania wajitokeze kuchangamkia fursa za ajira hizo.
Awali Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira ofisi ya Waziri Mkuu amesema kwamba mchakato wa kuwapata Watanzania wapatao 408 ulikuwa wa kuwashindanisha hivyo waliopata nafasi za ajira wataenda kuiwakilisha vyema nchi ya Tanzania nakuwezesha kupata mafanikio makubwa kiuchumi.