N Shomari Binda-Musoma
UMOJA wa Wanawake (UWT) wilaya ya Musoma mjini imetembelea gereza la wilaya ya Musoma na kutoa misaada ya kijamii.
Akizungumza na Mzawao Blog Katibu wa UWT wilaya ya Musoma mjini Angel Semwanza amesema huo ni mwendelezo wa matukio ya wiki nzima kuifikia jamii.
Amesema yapo matukio ambayo yamekuwa yakifanywa na kila Kata kupitia UWT ikiwemo kufanya usafi kwenye zahanati na vituo vya afya kwenye maeneo yao.
Angel amesema kufika kwenye gereza la Musoma ni sehemu ya watu wenye uhitaji na UWT Musoma mjini imetekeleza moja ya jukumu lao.
Amesema katika gereza hilo wamewafikia pia wafungwa na mahabusu wanawake na kutoa misaada ikiwemo mafuta,mchele,sukari na mahitaji mengine.
Katibu huyo wa UWT wilaya ya Musoma mjini amesema kuelekea kilele cha maadhimisho hayo ya wiki ya UWT Siku ya jumamosi yapo matukio yatakayofanyika ikiwemo mkutano wa hadhara.
Amesema moja ya matukio kabla ya tukio la mwisho la mkutano wa hadhara ni pamoja na kufika kwenye shule ya sekondari ya wasichana ya Songe na kuzungumza na wanafunzi pamoja na kugawa taulo za kike.
“Kesho kwenye kilele yapo matukio yatakayoanza mapema kuanzia saa 2 asubuhi hivyo tunawaomba wanawake na wana CCM wote kujitokeza kwenye matukio yote”
“Wiki nzima ya maadhimisho tumeifikia jamii na kutoa misaada ya kibinadamu na kufanya usafi na hii ndio thamani ya kuwepo kwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)” mesema Angel.