Watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta. Ushauri huu umetolewa leo Mei 17, 2024 na TMA kutokana na uwepo wa kimbunga “IALY” katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.
Mamlaka hiyo imeeleza kuwa mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kitaendelea kusalia katika Bahari ya Hindi katika eneo kati ya Madagascar na visiwa vya Shelisheli kwa siku nne zijazo kabla ya kuanza kupungua nguvu. Hii inamaanisha kuwa, kwa sasa, kimbunga hicho hakitarajiwi kuwa na athari za moja kwa moja katika kusababisha ongezeko la mvua nchini kutokana na umbali wake.
Hata hivyo, TMA imeonya kuwa vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa vinaweza kujitokeza katika Bahari ya Hindi. Hivyo, watumiaji wa bahari, wakiwemo wavuvi na wasafiri, wanashauriwa kuwa waangalifu na kuzingatia tahadhari zinazotolewa.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi. Ni muhimu kwa wananchi kuendelea kuwa makini na kuendelea kufuatilia taarifa na miongozo inayotolewa mara kwa mara na mamlaka hiyo ili kuepuka athari zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.