Na Shomari Binda-Musoma
UTEKELEZAJI wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ( CCM) ya mwaka 2020 hadi 2025 kwenye jimbo la Musoma mjini imetajwa kuwapa ushindi wenyeviti wa mitaa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024.
Hayo yamesemwa na mbunge wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo kwenye kikao na wenyeviti wa mitaa 73 katika kuzungumzia shughuli za maendeleo.
Amesema maendeleo kwenye sekta ya elimu,maji,afya,mundombinu imefanyika na hiyo itakuwa fursa ya kuwadanya wenyeviti wa mitaa kushinda.
Mathayo amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwenye maeneo hayo na utekelezaji umefanyika.
Amesema wenyeviti wa mitaa katika jimbo la Musoma mjini wanapaswa kutembea vifua mbele na kumsemea vizuri Rais Samia kwa kile alichokifanya.
Mbunge huyo amesema wakati wa sasa wenyeviti wa mitaa ni vyema wakawa na mahusiano mazuri na wananchi wanaowaongoza na kuwatatulia matatizo yao.
Amesema ni vyema pia kujiepusha na muingiliano wa shughuli za uongozi na kufanya vikao vya kuzungumzia maendeleo yaliyopatikana.
“Tumekutana hapa kwaajili ya kuzungumzia maendeleo kwenye mitaa yetu na ntaomba kila Mwenyekiti mwenye changamoto kwenye mtaa wake ntaomba azungumze changamoto kwenye mtaa wake.
“Rais Samia amefanya kazi nzuri kwenye jimbo letu na uchaguzi wa mwakani utakuwa mwepesi kwa sababu mengi tuliyo ahidi tumetekeleza“,amesema Mathayo.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mshikamamo A Christopher Sagi Korando amesema kwenye mtaa wake wananchi wameingia na kulima eneo la shule ya msingi Mshikamano nakuomba kero hiyo iweze kutatuliwa.
Pili Maregeri Mwenyekiti wa Mtakuja B pamoja na wenyeviti wengine wa mtaa ya mabondeni wameomba mitaro kwenye barabara iwekwe ili kukabiliana na mafuriko kwenye kipindi cha mvua.