Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (Katikati), akigonga kengele kuashiria kuorodhoreshsa rasmi kwa Hati Fungani ya Benki ya Azania ijulikanayo kama Bondi Yangu, katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Hafla iliyofanyika katika Ofisi za DSE, jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine aliziasa taasisi zingine kuiga mfano wa Azania ili uchumi uendeshwe kidigitali kwa kuuza hisa zao na kujiorodhesha katika Soko hilo. Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Azania, Mhandisi. Julius Ndyamukama (wa kwanza kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Dkt. Esther Mang’enya (wa pili kushoto), Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA), CPA Nicodemus Mkama (wa pili kulia), na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) Bw. Peter Nalitolela (wa kwanza kushoto).
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa tatu kulia) akifuatilia mbashara mnada wa Hati Fungani ya Benki ya Azania ijulikanayo kama Bondi Yangu, katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), baada ya hafla ya kuorodheshwa rasmi kwa Hati Fungani hiyo iliyofanyika katika Ofisi za DSE, jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine aliziasa taasisi zingine kuiga mfano wa Azania ili uchumi uendeshwe kidigitali kwa kuuza hisa zao na kujiorodhesha katika Soko hilo.
Serikali imezishauri taasisi mbalimbali nchini kujiorodhesha kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ili kutoa fursa kwa wananchi kushiriki kukuza uchumi wao binafsi na uchumi wa nchi kwa njia za kidijitali.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati wa hafla ya kuorodhoreshwa rasmi kwa Hati Fungani ya Benki ya Azania ijulikanayo kama Bondi Yangu, katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hafla iliyofanyika katika Ofisi za DSE, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa Uorodheshwaji wa Hatifungani hiyo utakuza ukwasi kwa wawekezaji kwa kutoa mwanya wa kuuza na kununua kupitia soko hilo na utaleta chachu kubwa katika kukuza Soko la Hisa la Dar es Salaam ambalo limekuwa mstari wa mbele katika kutoa fursa kwa watanzania kushiriki katika sekta rasmi ya fedha.
“Taarifa mbalimbali zilizotolewa zinaonesha mauzo ya Bondi Yangu yamekuwa ya mafanikio makubwa kwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 63.3 ambayo ni mafanikio ya asilimia 210.9, mafanikio ya namna hii ni nadra kwa mtoaji wa kwanza wa Hatifungani na hii inadhihirisha kuwa Benki ya Azania imeanza na mwanzo mzuri wa utoaji wa Hatifungani yake na malengo yao ni kukusanya zaidi ya TZS 100 bilioni ili kusaidia makundi ya wanawake, vijana na wajasiriamali wadogo kuweza kushirikishwa katika sekta rasmi ya fedha hapa nchini” alisema Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kuboresha mazingira ya kufanya biashara ili taasisi mbalimbali ziendelee kuja na ubunifu wenye tija ili kusaidia utoaji wa mikopo nafuu kwa makundi mbalimbali ya kinamama, vijana na wajasiriamali na kuleta chachu zaidi katika kuwawezesha wale ambao wanakwama kupata huduma rasmi za kibenki kuwezeshwa kiuchumi.
Aidha, Dkt. Nchemba alitoa wito kwa wananchi na wawekezaji kuchangamkia fursa ya awamu ya pili ya Hatifungani pale itakapozinduliwa rasmi ili kuongeza chachu ya maendeleo kwa taifa letu.
“Napenda kuwahakikishia wawekezaji na wananchi kwa ujumla kuwa Serikali yetu chini ya Uongozi mahiri wa Mama yetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta ya fedha na hasa kwenye masoko ya mitaji na dhamana” aliongeza Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Dkt. Esther Mang’enya, alisema kuwa hadi sasa jumla ya wawekezaji 650 wamefungua akaunti za CDS kuwawezesha kushiriki katika mauzo ya Bondi Yangu na shughuli zingine za masoko ya mitaji na dhamana ambapo zaidi ya asilimia 97.3 ya wawekezaji walioshiriki katika “Bondi Yangu” ni wawekezaji mmoja mmoja (retail investors).
Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, Bw. Peter Nalitolela, alisema kuwa thamani ya uwekezaji wa hatifungani katika soko hilo imeendelea kuongezeka na sasa imefikia takribani shilingi trilioni 27.6, huku idadi ya wawekezaji ikiwa imefikia 637,137.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, amepongeza mafanikio hayo, akibainisha kuwa yanatokana na mazingira wezeshi ya uwekezaji yaliyowekwa, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa kodi ya zuio kwenye faida ya hatifungani za taasisi.