Home Kitaifa ULEGA AKABIDHI MITUNGI YA MAJIKO YA GESI 1000 KWA WANAWAKE MKURANGA

ULEGA AKABIDHI MITUNGI YA MAJIKO YA GESI 1000 KWA WANAWAKE MKURANGA

NA SCOLASTICA MSEWA, MKURANGA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Abdallah Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga amekabidhi mitungi ya majiko ya gesi safi 1000 yenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 72 kwa makundi ya Wanawake wilayani Mkuranga kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kumkomboa mwanamke kutoka kwenye matumizi ya kuni na mkaa hadi kutumia gasi safi ambayo inatunza mazingira na kulinda afya ya binadamu.

Waziri Ulega amesema hayo wakati wa Kongamano la Wanawake Wilaya ya Mkuranga lililofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani ambapo Mgeni Rasmi katika Kongamano hilo, alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Wenye Mahitaji Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima.

Mheshimiwa Ulega kwa kushirikiana na Dkt. Gwajima wamekabidhi mitungi hiyo 1000 ya majiko safi ya kampuni ya Oryx kwa makundi ya Walimu wa kike wa wilaya hiyo, viongozi wanawake wa CCM na jumuhia zake, madiwani, Maafisa Ugani, Watendaji wanawake wa kata, Mamalishe na Wakuu wa idara za halmashauri.

Amesema kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuwa kinara wa kuwakomboa kina mama kiuchumi kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuwafanya waondokane na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yamekuwa na athari kwa mazingira na afya ya binadamu.

Amesema kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia alipokuwa kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP 28) uliofanyika Dubai mapema Mwezi Novemba, 2023, alitumia fursa hiyo kuielezea Dunia kuhusu dhamira yake ya dhati ya kuwawezesha Wanawake kujikwamua kiuchumi kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Aidha, kupitia Kongamano hilo, Waziri Ulega alimshukuru Mhe, Rais, Dkt. Samia kwa kumuongezea mitungi hiyo 500, huku akisema hatua hiyo inaonesha wazi dhamira yake ya kuwanusuru wakina mama na matumizi ya kuni na mkaa.

Amesema wanawake hutumia muda mwingi katika utafutaji wa kuni polini jambo ambalo huchelewesha harakati za maendeleo yao kwani hukutana na vikwazo na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchomwa miba, kugongwa na nyoka na hata mvua zinaponyesha pia kuni na mkaa haviwaki kwa urahisi kukwamisha kwa wanawake katika mapishi lakini majiko hayo yatakuwa msaada kwa akinamama hao na familia zao.

Naye, Mgeni Rasmi wa Kongamano hilo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Wenye Mahitaji Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amempongeza Mbunge na Uongozi wa Wilaya ya Mkuranga kwa hatua hiyo ya kuwawezesha kina mama nishati safi ya kupikia kwani ni njia moja wapo ya kuwakwamua kina mama hao kiuchumi.

Itakumbukwa kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa nchini Dubai katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP 28), pia alizindua Mradi wa Nishati Safi ya kupikia kwa lengo la kuwasaidia Wanawake Barani Afrika (AWCCSP)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!