Na Shomari Binda-Rorya
MBUNGE wa jimbo la Rorya Jafar Chege amemuomba Waziri wa Maji Juma Aweso kutuma timu kuhakikisha wananchi wa Kijiji cha Kinesi Kata ya Nyamunga wanapata huduma ya maji.
Chege ameyasema hayo leo februari 5 kwenye sherehe za miaka 48 ya Chama cha Mapinduzi ( CCM) zilizofanyika kwenye Kijiji hicho.
Amesema licha ya kuongelea jambo hilo bungeni ameona asisitize jambo hilo ili wananchi waondokane na adha ya maji.
Chege amesema amesikitishwa na kauli ya wananchi kusubili maji kwa kipindi cha zaidi ya miezi 8 kwa sababu ya kuharibika kwa pampu.
Amesema haikubaliki kuona kwa muda huo tatizo limeshindwa kupatiwa ufumbuzi na kupeleke wananchi kuchota maji ziwani yasiyo safi na salama.
” Hili jambo limenisikitisha kusikia wananchi wakilalamika kukosekana kwa maji kutokana na kuharibika kwa pampu licha ya mimi kulifanyia kazi muda mrefu.
” Nikitoka hapa ntaongea na Waziri Aweso aweze kutoa maelekezo na kutatuliwa tatizo ili kwa haraka na wananchi wa Kinesi wapate maji”,amesema.
Akizungumzia miaka 48 ya CCM Chege amesema maendeleo makubwa yamefanywa kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za elimu,afya,maji pamoja na miundombinu.
Amesema serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Dkt.Samia Samia Suluhu Hassan imemfanya mzazi wa jimbo la Rorya leo halipi ada shuleni huku shule mpya zikijengwa.
Chege amesema barabara zimefunguliwa na kuwafanya wananchi wa Rorya kufanya shughuli zao za kiuchumi na kujipatia kipato.
Amesema inaposherehekewa miaka 48 ya CCM yapo mazuri ya kujifunza na kuwaomba wananchi kuendelea kukiunga mkono chama hicho.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Mara Julius Masubo aliyekuwa mgeni rasmi kwenye sherehe hizo ametoa maagizo ya siku 7 zitumike kuhakikisha wananchi wa Kinesi wanarudishiwa huduma ya kupata maji.
Amesema miaka 48 ya CCM sìo ya wananchi kulalamika na kusema jambo hilo halikubaliki na kupongeza kazi nzuri iliyofanywa na serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuwahudumia wananchi.