Na Benny Mwaipaja, London
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameishukuru Taasisi ya Uingereza inayohusika na utoaji mikopo ya UK Export Finance (UKEF), kwa kukubali kufadhili ujenzi wa miradi kadhaa ya maendeleo nchini Tanzania ukiwemo mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba na ujenzi wa miundombinu ya barabara visiwani humo.
Dkt. Nchemba ametoa pongezi hizo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa UK Export Finance (UKEF), Bw. Tim Reid, Makao Makuu ya Taasisi hiyo, Jijini London, nchini Uingereza.
Alisema kuwa miradi hiyo, si tu kwamba itachokea shughuli za kiuchumi za visiwa hivyo ukiwemo utalii, bali pia itaboresha Maisha ya wananchi wa Tanzania kwa ujumla.
“Ninaishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuamua kutoa fedha za ujenzi wa miradi hiyo ambayo itasaidia kuboresha huduma za usafiri mijini na vijijini, itakuza uchumi, fursa za ajira na kuongeza kasi ya kuyafikia masoko, huduma za kijamii kupitia Sekta ya utalii” alisema Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba aliiomba taasisi hiyo, kuangalia uwezekano wa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha tano cha reli ya kisasa kinachoanzia Isaka hadi Mwanza chenye urefu wa kilometa 249 na miradi mingine ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa na Serikali ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuchochea maendeleo ya nchi.
“Mradi huu wa reli ni wa kimkakati na unatarajia kufungua milango ya kibiashara kwa kutuunganisha na nchi jirani za DRC Congo na Burundi, na umekusudiwa kuchochea pia biashara na maendeleo ya watu” alisema Dkt. Nchemba.
Naye, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, alisema kuwa wananchi wa Zanzibar, wanasubiri kwa hamu kuanza kwa ujenzi wa miradi hiyo ya upanuzi wa uwanja wa Ndege wa Pemba na ujenzi wa barabara za Unguja na Pemba, ambazo zitakuza shughuli za utalii na Maisha yao kwa ujumla
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa UK Export Finance (UKEF), Bw. Tim Reid, aliihakikishia Tanzania kupata fedha kwa ajili ya miradi hiyo lakini pia kuendelea kufadhili miradi mingine ya kimkakati itakayowasilishwa na Serikali ikiwemo maji na nishati.
Alisema kuwa hivi karibuni Taasisi hiyo itawaita wadau mbalimbali wakiwemo wawekezaji nchini Uingereza, na kuwaeleza kuhusu fursa zinazopatikana nchini Tanzania ili kuvutia mitaji na teknolojia mbalimbali zitakazo saidia kuongeza uzalishaji hususan katika sekta ya kilimo.
Uk Exporter Finance ni Wakala wa Serikali ya Uingereza inayojihusisha na kusaidia uagizaji na uingizaji wa bidhaa nchini humo kwa kutoa mikopo ya mitaji na kukatia bima bidhaa hizo lakini pia kuhakikisha kuwa zinakuwa na bei shindani kwenye masoko.
MWISHO