Na Scolastica Msewa, Chalinze.
Ujenzi wa kituo Cha kupoza umeme cha Chalinze na mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Julias Nyerere JNHPP hadi Chalinze utekelezaji wa jumla umefikia asilimia 86.23 ambapo 31 Desemba mwaka huu Umeme unatarajiwa kuwashwa ingawa mvua zinazoendelea kunyesha nchini kote zinakwamisha kazi hiyo.
Akitoa taarifa kwa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Pwani iliyofika kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa Kituo cha kupoza Umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Julias Nyerere Chalinze wakati wakiwa katika siku nne ya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika mkoa mzima wa Pwani.
Kaimu Meneja Mradi Eng. Fillipo Faraja Maliwa kukamilika kwa kituo hicho kitaboresha upatikanaji wa umeme kwenye Gridi ya Taifa na kuongeza hali ya ubora na uhakika wa upatikanaji wa umeme katika Gridi ya Taifa kwa kuunganisha umeme wa JNHPP kupitia kituo hicho cha kupoza umeme cha Chalinze.
Alisema ujenzi huo kwa upande wa usanifu umefikia asilimia 91.78 na usimikaji wa mitambo umefikia asilimia 81.18 kuhusu ununuzi wa vifaa umefanyika kwa asilimia 97.83 na majaribio ya ufanisi wafikia asilimia 29.47.
Alisema mpaka sasa zaidi asilimia 95 ya vifaa vyote vimeshawsili nchini ambapo Mradi huo unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.
Gharama za mradi huo mpaka kukamilika ni shilingi bilioni 128 ambapo shilingi bilioni 57.9 sawa na aslimia 54.2 zimekwishakulipwa hadi mwezi Novemba mwaka huu.
Akizungumzia mvua zinazoendelea kunyesha nchini na namna zinavyokamisha utekelezai wa ujenzi wa mradi huo Eng. Maliwa alisema mvua hizo zinakwamisha kazi zinazoendelea kwasasa katika kituo hicho ingawa wanajitahidi kupambana nayo kwa kuendelea na kazi huku mvua ikiendelea kunyesha.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha za kutekeleza mradi huo wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze ambao utakwenda kuongeza upatikanaji wa umeme nchini.
“Tuna matumaini nanyi sana kwamba ikifika mwezi Desemba 31 matumaini yetu ni kuona umeme haukatiki tena nchini kuanzia siku hiyo”
“Tumeona mitambo, tumeona kazi iliyofanyika na tumeona wafanyakazi tunawashukuru sana” alisema Mlao.
Aidha Mlao alimshukuru pia Rais Samia kwa ubora wa iradi ya sekta ya afya na elimu waliyoikagua na kusema serikali yaawamu ya sita inaboresha sekta ya afya na elimu kwa vitendo na kwa kuleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa wananchi wa Jimbo la Chalinze na Bagamoyo ambazo zimekuwa majibu ya kero za wananchi katika wilaya nzima ya bagamoyo.
Mlao amesema fedha hizo zimeleta suluhisho la changamoto zilizokuwa zikiikabili huduma ya afya katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo na kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule za Msingi Kiharaka na Bwilingu ambapo zimepatikana shule mbili mpya kupitia mradi wa BOOST.
Amewataka Walimu kufundisha kwa bidii ili waache alama ya matokeo mazuri ya ufaulu mkubwa yatakayoleta tija kwa Bagamoyo, Chalinze na Taifa kwa ujumla.
Aidha aliwapongeza Wabunge wa Majimbo ya Bagamoyo Mheshimiwa Muhalami Mkenge na Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, Wakurugenzi na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kwa usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo unaoipa CCM kutembea kifua mbele.
Alimalizia kwa kuwataka watumishi wa Halmashauri zote mbili kuendelea kuwa waaminifu na waadilifu kwa kutunza kile kinachopatikana kupitia mapato ya ndani.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Kamati hiyo ya Siasa iliweza kukagua miradi miwili ikiwa ni pamoja kutembelea Ujenzi wa Shule mpya ya awali na Msingi Kiembeni ambayo imejengwa kwa fedha za mradi wa Boost ambayo imesaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule ya msingi Kihalaka ambapo kuna wanafunzi zaidi ya 900 wamehamishiwa katika shule hiyo.
Akizungumzia Utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okashi amesema mpaka sasa tayari asilimia 98 ya ILANI imetekelezwa wilayani humo.
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Mheshimiwa Muhalami Mkenge ameiomba CCM Mkoa wa Pwani kusaidia upatikanaji wa majengo yanayomilikiwa na Hospitali ya Muhimbili yaliyoko karibu na Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ili yawe sehemu ya Hospitali hiyo katika kuwahudumia wananchi wa Jimbo hilo.Katika kuhitimisha,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Hassan Mwinyikondo alikishukuru Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani kwa ushirikiano wao wanaouonesha kwa Halmashauri hiyo katika kufanikisha Utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM.
Mwinyikondo alimalizia kwa kuahidi kuendeleza uaminifu na uadilifu kwa fedha za maendeleo ya miradi ya Serikali ili malengo ya kupitia CCM yatimie.
++++++++++++++++