NA Scolastica Msewa, Kibaha
Meneja wa kituo cha Uhakiki wa Vipimo Misugusugu Charles Mavunde amesema uhakiki wa matanki ya Malori ya kubebea vimiminika husaidia kurahisisha hata ukadiliaji wa bei za bidhaa na upatikanaji wa huduma katika kuwahudumia wananchi hivyo amewataka wenye malori hayo watoe ushirikiano wa kwenda kuhakiki ujazo wa matanki yao kila mwaka.
Akizungumza na waandishi wa Habari amesema iwapo muuzaji atauza kwa kipimo sahihi bila kupunjwa na mnunuzi akanunua kwa kipimo sahihi bila kupunjwa inampelekea hata anayepanga bei kwa mlaji wa mwisho kabisa ambaye ni mwananchi kupata nishati kwa bei rahisi isiyoumiza.
“Nitoe wito kwa bohari za mafuta, gesi na mafuta ya kula kuhakikisha kwamba wamezingatia Sheria ya Vipimo Sura 340 ili kila mteja anayehudumiwa tenki lake liwe limehakikiwa na Wakala wa Vipimo lina chati ya mwaka husika, stiki na nyaraka ambazo tunazitoa ili kuweza kuleta haki na manufaa kwa mlaji yaani mfanyabiashara, mnunuzi, wauzaji na wananchi kwa ujumla wanaohusika katika bidhaa hizo zinazobebwa katika matenki hayo”
“Kwahiyo lengo ni kumrahisishia mwananchi kupata huduma hizo kwa bei nafuu na kupatikana kwa uhakika na isiyo na maumivu katika kipengele cha bei”
“Wito katika sekta hii ya mafuta, gesi na mafuta ya kula ni kwamba matenki haya yanayobeba vimiminika hivo ni vipimo kabla ya kutumia wahakikishe kwamba bohari za vimiminika hivyo, wauzaji wa nishati hizo na watumiaji mmoja mmoja yaani wamiliki wa matenki haya wahakikishe kwamba kabla ya kuyatumia matanki hayo yawe yamehakikiwa katika kituo chetu au katika vituo vya mikoa niliyotaja”
“Lakini pia bohari zinazohusika kusambaza vimiminika hivyo wahakikishe kwamba wanasambaza vimiminika hivyo katika malori yenye matenki ambayo yamekwishahakikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo kwani kupokea na kumuuzia mteja kwa kutumia tenki ambalo halijahakikiwa ni kosa kwa mujibu wa Sheria Vipimo Sura 340 kwa hiyo kila mmoja azingatie ili tuweze kuinua uchumi wa nchi yetu uweze kuimarika zaidi” alisema Mavunde.
Alisema kituo cha uhakiki wa Vipimo Misugusugu Kibaha huhakiki matenki yabebayo vimiminika wastani wa 500 kwa mwezi ambapo uwezo wa kituo hicho ni kuhakiki malori 70 kwa siku ikiwa ni maboresho ya kutoka Wakala hao kupima malori 8 kwa siku katika mkoa wa Ilala jijini Dar es salaam lengo likiwa ni kumhakikishia vipimo sahihi kati ya mbebaji na mnunuzi wa kimiminika hicho.
Alisema kituo hicho kilianzishwa mwezi Machi mwaka 2019 ili kuhudumia malori yabebayo vimiminika ndani na nje ya nchi katika mataiafa ya Rwanda, Burundi, Malawi na DR Kongo.
Alisema kwa sasa wastani wa malori 30 huhakikiwa kwa siku katika kituo hicho ingawa kituo hicho cha Misugusugu kina uwezo mkubwa kuhakiki malori hadi 70 kwa siku ikiwa idadi hiyo hupungua kutokana na uwepo wa vituo vya uhakiki huo katika mikoa ya Iringa, Mwanza, mtwara na Arusha.
Mavunde alisema umuhimu wa uhakiki wa ujazo wa malori yabebayo vimiminika kuhakikiwa ni kumlinda mlaji yaani muuzaji, mnunuzi na mtumiaji wa nishati hiyo kwani lori linapokwenda kuchukua mafuta, gesi linatakiwa lijulikane ujazo wake sahihi.
“Kama lina ujazo wa lita 20000 mwenye kuuza mafuta aweze kuwa na uhakika kwamba kiasi cha mafuta anachojaza yawe ni lita 20000 na hata pata hasara kwa kupunjwa wala kumzidishia mnunuzi na mnunuzi pia kuwa na uhakika kwamba kiasi cha mafuta anachojaziwa kwenye tenki lake ni kimiminika sawa na kiasi kile sahihi”
“Lakini pia na mpokeaji wa kituo cha Mafuta anapoenda kumimina mafuta hayo awe na uhakika kiasi alicho letewa ni sahihi kwa kuendana na vipimo ambavyo anakuwa amepima tenki lake”
“Na kwa kufanya hivyo tunakuwa tumerahisisha utendaji wa biashara hii wa vimiminika ambayo ni muhimu katika uchumi wa nchi, tunajua nishati ya mafuta ni muhimu katika uchumi wetu na hata kupata takwimu inakuwa rahisi kama tuna vipimo sahihi”
“Tuna vipimo sahihi vya kupima mafuta kwaajili ya uhakiki wa malori ya vimiminika na katika uhakiki wa malori yabebayo mafuta ili mfanyabiashara aweze kupata faida na sio apate hasara kwa uzembe au matumizi yasiyosahihi ya vipimo nchini”
Amesema Wakala wa Vipimo wapo tayari kufanya kazi na wauzaji na wasambazaji wa mafuta na gesi kwamba wapo tayari kuendelea kushirikiana nao kutoa huduma kwa weledi na kwa wakati ili biashara zao ziweze kuleta manufaa kwa wafanyabiashara, mwananchi mmoja mmoja na kwa taifa zima ili tuweze kuimarisha uchumi wetu kwa mwananchi mmoja mmoja na kwa taifa kwa ujumla.
++++++++