Hatimaye Tani 3500 za ufuta zilizokwama kuuzwa tarehe 6 mwezi huu zimeuzwa mkoani Pwani Katika uzinduzi wa mnada wa zao la ufuta wa msimu wa mavuno ya mwaka 2024/2025 huko Wilayani Kibiti.
Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya uzinduzi huo huko Kibiti mkoani Pwani Meneja wa Chama kikuu Cha ushirika wa Wakulima wa mkoa wa Pwani Mantawela Hamisi amesema ufuta huo utauzwa kwa bei ya wastani wa shilingi 3653.21 baada ya kushindwa kufanyika kutokana na tatizo la kimfumo kutokea siku ya tarehe 6 mwezi huu.
Mantawela alisema kulitokea tatizo la kimfumo katika mfumo wa Soko la bidhaa Tanzania TMX na kusababisha ufuta huo kuto kuuzwa siku hiyo ya alhamisi lakini baada ya kuimarika mfumo huo na kufanyika kwa maandalizi mazuri mnada umefanyika juzi tarehe 8 siku ya jumamosi.
“Kama tulivyoona mnada huo umefanyika kwa mafanikio na wakulima wameridhia bei hiyo ya wastani wa shilingi 3653.21/- na tunatarajia bei kuendelea kupanda kadri tunavyoendelea kufanya minada zaidi katika msimu” alisema Mantawela.
Hata hivyo Mantawela amewashauri Wakulima na viongozi wa Vyama vya msingi vya kilimo AMCOS mkoani humo kuzingatia usafi wa zao hilo kabla ya kupeleka ghalani hata kupelekwa ghala kuu
“Kusafisha vizuri ufuta huo kutaongeza ushindani kwa wanunuzi na mwisho wa siku mkulima atapata bei kubwa ambayo itakithi tija ya mkulima aliyotumia kwenye kulima ” alisema Mantawela.
Aidha Mrajis msaidizi wa Vyama vya ushirika mkoa wa Pwani Abdillahi Mutabazi aliwataka wakulima, viongozi wa Vyama vya msingi vya ushirika na viongozi wa maghala makuu kuzingatia usafi na kufikisha ufuta kwa wakati ghala kuu.
“Bora uchelewe kufika sokoni lakini usafishe vizuri ufuta wako kwa kuzingatia usafi wa viwango vilivyokusudiwa na Soko la kitaifa na Kimataifa kuliko kuharakisha kufikisha ufuta sokoni bila kuzingatia usafi wa ufuta wako” alisema Mutabazi.