Fedha zilizotumika nchini kutokana na mauzo ya dhahabu zafikia shilingi Trilioni 5.6
Wajumbe wa Kamati wapongeza matokeo chanya ya ubia, yashauri maboresho
Kampuni yaanisha mpango wa kuongeza uhai wa migodi, uzalishaji, teknolojia za kisasa
Halmashauri 4 zanufaika kupitia ushuru wa huduma, CSR na Local Content
Dodoma
Twiga Minerals Corporation Kampuni ya ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick Gold Cooperation imeieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu mafanikio yaliyopatikana baada ya kuanzishwa kampuni hiyo kiasi cha shilingi trilioni 5.6 kimetumika nchini kutokana na mauzo ya dhahabu kupitia migodi yake huku shilingi trilioni 2.7 sawa na asilimia 48 zikitumika kwa wazabuni wazawa wanaotoa huduma mbalimbali katika migodi ya kampuni hiyo.
Akiwasilisha mada kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika semina ya siku moja kwa kamati hiyo Januari 29, 2023 jijini Dodoma, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Twiga Melkiory Ngido amewaeleza wajumbe wa kamati hiyo kuwa mwaka 2020, kampuni ya Twiga ilitoa gawio kwa serikali kiasi cha dola za Marekani milioni 250 huku katika kipindi cha mwaka 2017- 2022, kiasi cha shilingi bilioni 24.3 kikitolewa kwa halmashauri kama tozo mbalimbali zinatozwa katika maeneo yanakofanyika shughuli za madini kupitia migodi yake.
Pia, amesema kwamba, kiasi cha shilingi bilioni 23.5 kimewekezwa katika miradi mbalimbali ya kijamii katika sekta za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara na mingine . Amezitaja Halmashauri ambazo zimenufaika kutokana na uwepo wa migodi hiyo kuwa ni pamoja na Kahama, Nyang’hwale, Msalala na Tarime kupitia migodi yake ya Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara.
Akizungumzia nafasi ya ushiriki wa Watanzania katika migodi ya kampuni hiyo, amesema, asilimia 96 ya watanzania wameajiriwa katika migodi hiyo, asilimia 45.3 ni ajira mpya za watanzania wanaotoka katika maeneo yanayozunguka migodi hiyo, asilimia 11 ni ya wafanyakazi wanawake na asilimia 57 ni watanzania walio katika ngazi za maamuzi.
Kuhusu mipango ya kuendeleza kampuni, amesema kampuni ya Twiga imepanga kuendeleza shughuli za utafiti ili kuongeza uhai wa migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu na matazamio ni uhai wa migodi kufikia mwaka 2040 kwa mgodi wa Bulyanhulu na mwaka 2039 kwa mgodi wa North Mara.
‘’ Tunaendelea kuwekeza kwenye utafiti na matarajio yetu ni uhai wa migodi yetu ni kufikia mwaka 2050. Tumewekeza kwenye tekinolojia za juu na za kisasa kuwahi kutokea ambazo zinawezesha kuongeza uzalishaji bila kuhatarisha maisha ya wafanyakazi,’’ amesema Ngido.
Pamoja na kueleza mafanikio hayo, amesema zipo changamoto kadhaa ambazo ameiomba serikali na Bunge kusaidia ili kuweza kuzitatua ikiwemo changamoto ya fidia kwa baadhi ya watu wanaofanya tabia ya tegesha.
Kutokana na mafanikio hayo yaliyopatikana kupitia ubia huo, mfumo wa ubia umetajwa kuwa ni wa mfano kuwahi kutokea katika historia ya sekta ya madini duniani ambapo Kampuni inatarajia kutumia mfano wa ubia wa Tanzania na Barrick kwa ajili ya manufaa ya nchi ambako Barrick Corporation imewekeza katika migodi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dunstan Kitandula amepongeza kutokana na kiwango kikubwa cha ushiriki wa watanzania katika shughuli za kampuni hiyo na kuwataka wote walioaminiwa kushika nafasi za juu kutanguliza mbele maslahi ya taifa.
Aidha, ameitaka Wizara ya Madini kulichukulia kwa umuhimu na ukaribu suala ambalo linahusu jambo lolote linaloharibu taswira ya sekta ya madini nchini.
Awali, akizungumza katika semina hiyo, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kampuni hiyo imetoa wasilisho katika semina hiyo ili kuitaarifu kamati kuhusu hatua mbalimbali zilizofikiwa tangu kuanzishwa kwa kampuni husika na kuongeza kwamba, wizara inaendelea kuhakikisha kwamba Sekta ya Madini inaendelea kuchangia ipasavyo katika pato la taifa ili ifikapo mwaka 2025 iweze kufikia lengo la asilimia 10.
Mbali na Kamati ya Bunge, semina hiyo imehudhuriwa na wajumbe wa menejimenti na wataalamu kutoka Wizara ya Madini na wataalam watendaji kutoka taasisi yake ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Tume ya Madini na Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI)