Kampuni ya Mo Geen International Sports Promotion imeandaa pambano la ndondi mkoani Morogoro ikiwashirikisha mabondia nyota wenye historiia mbalimbali ndani na nje ya nchi, pambano ambalo litapigwa Novemba 25 mwaka huu.
Akizungumza leo Oktoba 12,2022 na Waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Afisa Uhusiano wa Kampuni ya Mo Geen International Bw.Kessa Mwambeleko amesema mabondia takribani sita wataweza kushiriki siku hiyo akiwemo Twaha Kiduku, Dulla Mbabe na Karim Mandonga ambapo wote hao wamepewa muda wa kuelezea walivyojipanga na wote wapo tayari kwa pambano na kuwapa wananchi burudani.
“Bondia nyota Twaha Kiduku, ambaye ana historia kushinda mikanda mbalimbali, atapambana na Bondia Damian Bonell kutoka nchini Argentina ambaye pia ana historia ya kusisimua kwenye tasnia ya ngumi”. Amesema
Amesema Pambano lingine katika siku hiyo litawahusisha mabondia Dulla Mbabe ambaye mashabiki wake walikuwa na kiu ya kumuona ulingoni kwa muda mrefu, akipambana na bondia Mkongo, Mbiya Kanku.
Aidha pambano lingine litamhusisha bondia aliyejipatia umaarufu mkubwa katika siku za hivi karibuni, Karim Mandonga atakayepambana na Bondia Said Mbelwa.
Nae Bondia Twaha Kiduku amewataka wapenzi ngumi waweze kushiriki kushuhudia burudani nzuri kutoka kwake na kuwahakikishia mashabiki ushindi dhidi ya mpinzani wake Muargentina Damian Bonell.
Pamoja na hayo ameupongeza uongozi wa kampuni ya Mo Geen International Sports Promotion kwa kuandaa pambano hilo ili mabondia wengine waweze kuonesha vipaji vyao katika tasnia ya ngumi na kuweza kupeperusha bendera ya taifa.
Kwa upande wake Karim Mandonga amesema atahakikisha anashinda pambano hilo na kumtambia mpinzani wake kuwa atampiga na kutoa burudani kwa mashabiki wake ambao wamekuwa wakimshangilia.