NA. MWANDISHI WETU
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga aemtoa wito kwa wadau kuendelea kuunga mkono watu wenye ulemavu nchini katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuwapatia vifaa saidizi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kujiletea maendeleo yao.
Ameyasema hayo Novemba 22, 2023 wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu katika Mkoa wa Mtwara vilivyotolewa na Kampuni ya Sigara ya TCC ikiwemo fimbo nyeupe, vyereani, baiskeli na viti mwendo kwa lengo la kuwasaidia katika na kuyafikia mahitaji waliyonayo.
Naibu Waziri Ummy alisema kuwa kundi la wenye ulemavu ni vyema lisiachwe nyuma kwa kuzingatia mchango wao katika jamii hususan katika shughuli mbalimbali ikiwemo za kiuchumi.
“Watu wenye ulemavu tunamahitaji mengi, hiki kilichofanywa leo na kampuni ya Sigara kimenifurahisha sana na mmeonesha namna gani mnajali na mmiunga Serikali mkono kwa vitendo, na mmegusa kundi hili Muhimu, niwaombe na wadau wengine kufanya kwa kuzingatia mahitaji yao,” alisema Mhe Nderiananga.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed aliupongeza uongozi wa Kampuni ya Sigara kwa kuendelea kuwakumbuka watu wenye ulemavu huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha hakuna kundi linaliloachwa nyuma kwa lengo la kuendelea kuchangia katika shughuli za kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
“Ninawashukuru wadau wetu Kampuni ya Sigara kwa kuona umuhimu wa kuwakumbuka watu wenye ulemavu, sisi Mkoa tumefarijika sana kwa mchango wenu endeleeni kufanya hivyo kwa makundi yenye mahitaji,” alieleza Kanali Abbas
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Watu wenye ulemavu Mtwara akitoa shukrani kwa niaba ya viongozi wa SHIVYAWATA mkoa Bi. Zamda Said alipongeza Kampuni ya Sigara kwa kuwasaidia vifaa hivyo huku akitumia nafasi hiyo kuwaasa watu wenye ulemavu kuvitunza vifaa hivyo na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Msiuze vifaa hivi, tuvitumie kwa manufaa yetu na wengine, ili inapotokea wadau wanajitokeza kutusaidia wasikatishwe tamaa kwa kutokutunza vifaa husika,” alisema Bi. Zamda.
=MWISHO=