Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema TRA itaendelea kusimamia ustawi wa biashara nchini kwa kuhakikisha kuwa hakuna biashara inayokufa ili uchumi wa nchi uendelee kuimarika.
Akizungumza na Wafanyabiashara mkoani Singida Februari 05.2025 Kamishna Mkuu wa TRA amesema miongoni mwa majukumu ya TRA ni kuwezesha ukuaji wa biashara na kusaidia kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji wa nchini.
“Bila nyie Wafanyabiashara sisi TRA hatuwezi kuwepo, ninyi ni watu muhimu sana kwetu na ndiyo maana Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametupa jukumu la kuzilunda biashara zisife ili tuendelee kukusanya Kodi” Kamishna Mkuu Mwenda.
Kamishna Mkuu Mwenda amewaagiza Mameneja wa TRA mikoa yote kutatua kwa wakati changamoto zinazowakabili Wafanyabiashara kwenye maeneo yao na kusajili Walipakodi wapya ili kuongeza wigo wa ukusanyaji Kodi hali itakayosaidia kupunguza viwango vya kodi na kuleta usawa katika ushindani wa biashara.
Amesema ni jukumu la kila mmoja kuwafichua watu wanaokwepa Kodi maana vitendo hivyo vinaathari kwa kila Mwananchi kutokana na kukwamisha shughuli za maendeleo na kuwanyonya wachache wanaolipa Kodi hali ambayo inahatarisha usalama wa biashara.
Akiwa mkoani Singida Kamishna Mkuu wa TRA alitoa tuzo kwa Walipakodi waliofanya vizuri kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na kuwataarifu kuwa kuanzia mwaka wa fedha ujao tuzo hizo zitakuwa ni Tuzo za Rais ili kuonyesha umuhimu wa Mlipakodi nchini.
Bw. Mwenda amesema TRA itaendelea kutoa elimu ya Mlipakodi kwa Wafanyabiashara na watoa huduma ili kila mmoja afahamu wajibu wake katika ulipaji wa Kodi.