Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa rai kwa wafanyabishara nchini kutumia maonesho ya kibiashara ya kimataifa ya sabasaba sambamba na fursa za makampuni ya kigeni ili kujifunza na kujipanga kuhudumia masoko makubwa ya ndani, kikanda na kimataifa.
Amesema kufunguka kwa Soko la Eneo Huru la Afrika – AfCFTA ambalo linakadiriwa kuwa na walaji zaidi ya bilioni 1.3 kutoka nchi 53 barani Afrika ni fursa kubwa kwa wafanyabiashara wa Tanzania.
“niwaombe wale wote wenye bidhaa zenye viwango na wanaoweza kukidhi vigezo kujisajili kupitia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ili kunufaika na mpango huo. Ni muhimu sana tukaweka jitihada za dhati kuyafikia masoko haya na siyo kuwa waangaliaji tu na kulalamika.“
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Julai 05, 2023) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa maonesho ya biashara ya kimataifa ya 47, Temeke Dar es Salaam.
Aidha, amezitaka Wizara za Uwekezaji, Viwanda na Biashara ishirikiane na Wizara ya Kilimo katika kuandaa mpango wa pamoja kuhakikisha uzalishaji unafanyika kwa kuzingatia mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Wizara hizi mbili lazima zisomane kiutendaji. Aidha, wataalam wa TanTrade washirikishwe kikamilifu katika kutekeleza majukumu ya utafutaji na ufunguaji wa fursa za masoko ndani na nje ya nchi.”