Home Biashara TUME YA MADINI YAJA NA MIKAKATI MIPYA YA UKUSANYAJI WA MADUHULI

TUME YA MADINI YAJA NA MIKAKATI MIPYA YA UKUSANYAJI WA MADUHULI

Yapitisha maombi mapya 7596 ya leseni za madini kuanzia Julai hadi Septemba, 2023

Mhandisi Samamba awataka watanzania wengi kuwekeza kwenye Sekta ya Madini

Ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanywa na Serikali ikiwa ni pamoja na kufanya Marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Mabadiliko hayo yalifanyika Mwaka 2017 yalipelekea kuanzishwa kwa Tume ya Madini na kuvunja Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na TANSORT.

Akielezea uanzishwaji wa Tume ya Madini kwa kifupi Katibu Mtendaji wa Tume, Mhandisi Yahya Samamba anaeleza kuwa, Tume ya Madini ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kama ilivyorekebishwa mwaka 2017 lengo likiwa ni kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Sera na Sheria ya Madini ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.

Akielezea majukumu ya Tume ya Madini kwa ujumla wake, Mhandisi Samamba anafafanua ni pamoja na kutoa na kusimamia leseni za madini, kusimamia shughuli za utafutaji, uchimbaji, na biashara ya madini, kusimamia ukaguzi wa migodi na mazingira kwa ujumla.

Akielezea mikakati iliyowekwa na Tume ya Madini katika kuhakikisha Sekta ya Madini mchango wake kwenye Pato la Taifa unaendelea kukua na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025, Mhandisi Samamba anasema kuwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha wananchi wengi kushiriki kwenye uwekezaji katika Sekta ya Madini, kuanzia kwenye uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.
Anaendelea kusema kuwa elimu inayotolewa kuhusu fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini kupitia mikutano, majukwaa, warsha na maonesho mbalimbali yanayofanyika kuanzia kwenye ngazi ya kimkoa na kitaifa imeleta matokeo makubwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa maombi ya leseni za madini.

Anafafanua kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Septemba, 2023 Tume ya Madini ilipokea maombi mapya ya leseni za madini 7596 ambayo yote yaliidhinishwa baada ya kukidhi vigezo.

“Bado tunaendelea na uhamasishaji wa wachimbaji wa wadogo wa madini wasio rasmi kuwafanya rasmi kwa kuwasajili sambamba na kutatua changamoto zinazowakabili ili uchimbaji wao ulete tija huku Serikali ikipata kodi zinazotumika katika uboreshaji wa huduma za jamii,” anasisitiza Mhandisi Samamba.

Akielezea mikakati mingine inayotekelezwa na Tume, Mhandisi Samamba anagusia namna uhamasishaji unavyofanywa katika migodi ya madini katika utekelezaji wa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini ambapo kumekuwepo na mwitikio mkubwa sana wa ushiriki wa wananchi kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.

“ Kwa mfano katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, 2023 Tume ilipokea mipango ya ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini 234 ambapo mipango 232 ilipitishwa baada ya kukidhi vigezo,” anasisitiza Mhandisi Samamba.

Akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli katika kipindi husika, Mhandisi Samamba anaendelea kusema kuwa kati ya kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, 2023, Tume ya Madini ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 184.53 na kusisitiza kuwa Tume kupitia Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa imeendelea kuweka mikakati kabambe ili kuhakikisha lengo ililopewa la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 882.12 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023-2024 linafikiwa.

Hata hiyo anaainisha kuwa Tume ya Madini imeweka mikakati ya kuhakikisha wachimbaji wa madini nchini wanaendesha shughuli zao kwa usalama kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara na kutoa elimu juu ya uchimbaji salama usioathiri afya na mazingira sambamba na kuepuka ajali zinazoweza kujitokeza migodini.

“ Kwa mfano katika kipindi cha robo mwaka, Tume ilifanya ukaguzi ili kutathmini eneo lililopendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la topesumu kwenye migodi au mitambo ya uchakataji wa madini katika miradi ya Green Pacific Investment Limited katika Kijiji cha Mbangala, Wilaya ya Songwe Mkoani Songwe; Adam Thomas Mungirwa katika Kijiji cha Mtakuja, Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi; Kampuni ya Mwaloni Limited iliyopo Wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara; Hexad Company Limited na Nyati Gold Mine katika Mkoa wa Geita na Msalala Gold Mine Ltd iliyopo Kahama, Mkoani Shinyanga,” anasisitiza Mhandisi Samamba.

Anaongeza kuwa pia ulifanyika ukaguzi kwa ajili ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa mabwawa ya topesumu katika miradi ya Lindi Jumbo na Uranex mkoani Lindi; Taur Tanzania Limited katika Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora; na Mgodi wa Peponi Mkoani Singida kwa lengo la kuangalia uzingatiaji wa Sheria ya Madini Sura ya 123 na kanuni zake.

Aidha, Mhandisi Samamba anahitimisha kwa kuwataka wadau wa madini nchini kufanya shughuli zao kwa uzalendo, kufuata sheria ya madini na kanuni zake sambamba na kujiepusha na vitendo vya utoroshaji wa madini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!