Na Monica Sibanda – Dodoma
Afisa uhusiano wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Esta Mbanguka, ametoa wito kwa wakulima wanaotembelea viwanja vya Nanenane na wakulima wa nchi nzima kutumia huduma za mtandao zinazotolewa na shirika hilo ili kuboresha kilimo na kuendana na teknolojia.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 03 katika viwanja vya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma, Esta amesema wamewaletea wananchi huduma za kidigitali ikiwemo “Fiber Mlangoni” ili kuhakikisha huduma hizo zinapatikana katika maeneo yote ya nchi na kwa kila sekta ikiwemo kilimo na uvuvi.
“Tumewaletea mifumo ya teknolojia wakulima na ambao sio wakulima kwani sasa hivi dunia yote ipo kidigitali. Sasa watakaofanya kilimo ni lazima wauze au watafute pembejeo za kilimo. Wanapokuwa na huduma ya mtandao wanaweza kuwafikia wauzaji wa pembejeo na pia wanunuzi wa mazao yao kwa njia rahisi,” amesema Esta.
Pia ameongeza, wateja wao nchi nzima wanashauriwa kutoa taarifa katika kituo cha huduma kwa wateja pindi wanapopata changamoto yoyote wanapotumia huduma zao ili zitatuliwe kwa wakati.
“Nitoe rai kwa wateja wote nchini kuripoti kituo cha huduma kwa wateja pindi wanapopata changamoto katika huduma zetu ili tuweze kuwasaidia kwa haraka. Lakini wanapokuwa wanazungumza pembeni wanabaki na tatizo na sio kutatua tatizo,” amesema Esta.