WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka miwili imetumia shilingi trilioni 1.29 kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Amesema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 454.3 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za elimu ya awali na msingi ambapo jumla ya shule mpya zilizojengwa ni 342, vyumba vya madarasa 9,189, nyumba za walimu 346, mabweni 28 na ukarabati wa shule kongwe 45.
Amesema hayo leo (Alhamisi, Februari Mosi, 2024) Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Taarifa kuhusu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na Mitaala ya Elimu ngazi ya Elimu Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Amesema utekelezaji wa mtaala mpya umeanza katika ngazi ya Elimu ya Awali, Elimu ya Msingi – Darasa la I na III, Elimu ya Sekondari Kidato cha Kwanza katika baadhi ya fani za amali katika shule 96 za Serikali na Binafsi ambazo zina miundombinu wezeshi kama karakana na Walimu wa fani hizo.
Mheshimiwa Majaliwa amesema shilingi bilioni 837.8 zimetolewa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zimetumika katika ujenzi wa shule za Sekondari mpya 486, vyumba vya madarasa 21,990, nyumba za walimu 280, mabweni 221, ukarabati wa shule kongwe 21, maabara 151 na mabwalo 23.
Aidha, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha hizo zilizoboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia shuleni ambazo zimeongeza udahili wa wanafunzi wa elimu ya awali msingi na sekondari pamoja na kuimarika kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne.
“Nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono yake juu ya Taifa hili hususan katika suala la elimu. Tutakumbuka wote kwamba tarehe 22 Aprili, 2021 ndani ya Bunge hili, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo ya kufanya mabadiliko katika mfumo wa elimu ulioko nchini.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema jambo hilo limeakisi mawazo ya Waheshimiwa Wabunge ambayo kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiishauri Serikali, kutokana na maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Serikali imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo kupokea maoni, kuyachambua na kuanza utekelezaji baada ya kufanya maboresho.
Waziri Mkuu amesema Serikali kwa kushirikiana na walimu na wadau wa elimu nchini ilijiwekea mikakati ya kuboresha elimu ya msingi na sekondari ambapo vigezo mbalimbali viliwekwa na vilianza kutekelezwa Januari, 2023 ili kuboresha elimu ya msingi na sekondari.
“Nawapongeza viongozi wote wa Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kubuni na kusimamia utekelezaji wa mikakati hii ya kuboresha elimu ya msingi na sekondari ambayo imeanza kuonesha mwelekeo mzuri. Aidha nawapongeza viongozi wa ngazi ya Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata na Shule pamoja na Walimu na Wazazi kwa kushirikiana vema katika kutekeleza mikakati hii ya kuboresha elimu likiwemo suala la upatikanaji wa chakula cha wanafunzi shuleni kwa ufanisi mkubwa.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezielekeza Ofisi ya Rais–TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zihakikishe wanafunzi wote wenye rika legwa wanaandikishwa shuleni kwa wakati, ziendelee kusimamia udhibiti wa michango holela shuleni pamoja na kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya mafunzo ya utekelezaji wa mtaala mpya na kuzitumia kama ilivyokusudiwa.
Mbali na maelekezo hayo, pia Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania wote wahakikishe wanafunzi wote wenye umri wa kujiunga na elimu ya awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza wanadahiliwa na kuanza masomo mara moja. “Ninatoa rai kwa viongozi wote kuendelea kuwasimamia walimu kwa upendo na uadilifu ili kuwatia moyo na kuongeza ari ya uwajibikaji na kuleta matokeo chanya ya ufundishaji na ujifunzaji.”