Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kushirikiana na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kutoa Elimu ya Kodi ili kuhamasisha Wananchi kulipa kodi kwa hiari.
Hayo yamebainishwa wakati wa mazungumzo baina ya Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda alipomtembelea na kufanya mazungumzo na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dr. Sheikh Abubakar Ali Zubeir kwenye Ofisi za BAKWATA Jijini Dar es Salaam.
Wakati wa mazungumzo yao Kamishna Mkuu Mwenda amesema licha ya kwenda kumtakia Heri ya Mwaka Mpya Mufti pia ameenda kuomba ushirikiano katika eneo la Elimu kwa Mlipakodi ili kuwezesha kuongeza uelewa zaidi wa masuala ya Kodi kwa jamii.
Amesema kuwa TRA itatoa Elimu ya Kodi kwa Viongozi wa Dini zote kwa Nchi nzima ili pawepo na uelewa wa pamoja utakaosaidia Viongozi hao kufikisha elimu hiyo kwa waumini wao.
“Suala la Kodi ni la kiibada hivyo kuhamasisha Kodi ni kuhamasisha Ibada jambo ambalo ni jema na linasaidia katika maendeleo ya nchi” amesema Kamishna Mkuu Mwenda.
Bw. Mwenda amesema faida za Kodi ni za moja kwa moja maana Watoto wanasoma shule bure, hospitali zinajengwa, barabara zinajengwa hayo ni miongoni mwa matunda ya Kodi.
Kwa upande wake Mufti Dk. Zubeir amesema wapo tayari kushirikiana na TRA katika masuala ya elimu ambapo watakaa na watumishi wa TRA na kupanga namna nzuri ya kufikisha elimu ya masuala ya Kodi kwa waumini wao.
Dk. Zubeir amesema iwapo Masheikh watapatiwa elimu ya Kodi itawawezesha kuandaa mihadhara na kutoa elimu kwa waumini wao huku akidokeza kuwepo kwa mpango wa kuandika kitabu kuhusu masuala ya Kodi.
“Hili jambo limekuja muda muafaka kabisa, tupo tayari kuwaandaa watu wetu kwa utaratibu tutakaokubaliana na TRA ili elimu ya Kodi iende kwa waumini na bahati nzuri jambo hili hata kwenye vitabu vya dini limo, maana hata Sisi huku misikitini huwa tuna Zaka hivyo ni Vema kila mmoja atambue wajibu wake katika kupia Kodi” amesema Mufti Dk. Zubeir.
Amesema kuwa katika siku za karibuni wameshuhudia utendaji mzuri wa TRA ambao umeongeza makusanyo ya Kodi.