Home Kitaifa TRA KUONGEZA IDADI YA WAENDESHA UCHUMI WALIOIDHINISHWA

TRA KUONGEZA IDADI YA WAENDESHA UCHUMI WALIOIDHINISHWA

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ipo katika mkakati wa kuongeza idadi ya Waendesha Uchumi Walioidhinishwa (Authorized Economic Operators (AEO)) ili kuongeza kasi ya uendeshaji wa shughuli za Uchumi nchini ikiwemo uondoshaji mizigo Bandarini na usafirishaji kwenda nchi jirani.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vyeti kwa AEO 5 zilizopatiwa leseni msimu huu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema idadi ya AEO iliyopo nchini haitoshi ikilinganishwa na idadi ya Watanzania.

Amesema kwa sasa nchini zipo jumla ya AEO 41 idadi ambayo haitoshi, hivyo ipo haja ya kuongeza idadi ambapo TRA kwa kushirikiana na Waendesha Uchumi Walioidhinishwa watakuja na Kampeni ya kuhamasisha wadau wengine wa sekta hiyo kusajiliwa.

“Tunataka tuongeze zaidi idadi ya AEO zinazotoa huduma ili biashara zichangamke na kodi zilipwe vizuri zaidi, hawa wakiwa wengi Bandarini, mipakani na katika sekta mbalimbali ikiwemo usafirishaji kutachangamka” amesema Bw. Mwenda.

Ameeleza kuwa TRA ipo kuwasaidia Waendesha Uchumi Walioidhinishwa hivyo itahakikisha wanapata faida zote zinazotoka na kuidhinishwa kama ilivyo kwa wenzao waliopo nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Bw. Mwenda amesema Mapato ya TRA kwa Asilimia zaidi ya 40 yanachangiwa na Bandari na kwa upande wa Bandari Waendesha Uchumi Walioidhinishwa wanachangia Asilimia zaidi ya 70 hivyo ni wadau muhimu kwa Uchumi wa Nchi.

Kwa upande wake Kamishna wa Forodha Bw. Juma Bakari akizungumza katika hafla hiyo amesema wamekuwa wakisimamia usalama na kodi kwa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini ambapo wamekuwa wakitoa leseni kwa Waendesha Uchumi wanaovuka mipaka ili waidhinishwe.

Amesema kumekuwa na faida nyingi wanazopata Waendesha Uchumi Walioidhinishwa ambazo zinarahisisha utendaji kazi wao tofauti na wale wasioidhinishwa.

Kwa upande wake mwakilishi wa Waendesha Uchumi Walioidhinishwa kutoka AFT Bw. James Mramba amesema mpango wa kusajiliwa umekuwa na manufaa kwao na umekuwa ukiwasaidia kupunguza changamoto katika utendaji kazi wao.

Amesema uaminifu ndiyo Nguzo kubwa katika kazi zao na kutoa wito kwa wengine ambao bado hawajasajiliwa kwenye mfumo huo, kujisajili ili kurahisisha kazi zao.

AEO zilizopatiwa vyeti ambazo ni 1. Jambo Food Products 2. Coca cola Kwanza Ltd 3. Puma Energy 4. Gupiter Auto Spares and Hardware Ltd 5. Sun Flag Tanzania Ltd tayari zimeshasajiliwa na TRA na kupatiwa leseni.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!