Home Kitaifa TMA YATAHADHARISHA MVUA KUBWA MIKOA YA TANGA, PWANI, DAR ES SALAAM NA...

TMA YATAHADHARISHA MVUA KUBWA MIKOA YA TANGA, PWANI, DAR ES SALAAM NA VISIWA VYA UNGUJA, TABORA NA KIGOMA

Na Magrethy Katengu

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka ambayo ni mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma na na Kusini mwa Morogoro. Taarifa hiyo imesema kipindi cha nusu ya msimu (Novemba 2023 hadi Januari, 2024) kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi ukilinganisha na nusu ya pili (Februari hadi Aprili 2024), uwepo wa El-Niño unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za Msimu.

“Mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Iringa, Lindi, Mtwara, Singida, Dodoma, kaskazini mwa mkoa wa Katavi, Kigoma na Tabora. Aidha, mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa kusini mwa mkoa wa Katavi, mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya na Ruvuma”. Alisema Dkt. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA na Makamu Mwenyekiti Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia Nchi (IPCC) wakati wa mkutano na vyombo vya habari kuhusiana na mwelekeo wa mvua za Msimu, katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam,Tarehe 31 Oktoba, 2023.

Dkt. Chang’a alibainisha athari zinazoweza kujitokeza ikiwa ni vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo, vile vile, kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka, aidha, Dkt. Chang’a alitoa ushauri kwa wadau mbalimbali kuzingatia matumizi endelevu ya uhifadhi wa rasimali maji.

Katika hatua nyingine, Dkt. Chang’a alifafanua kuwa Msimu wa Vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba, 2023 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia) pamoja na Zanzibar (visiwa vya Unguja na Pemba) utabiri wake ulitolewa tarehe 24 Agosti, 2023. Mvua hizo zimeshaanza katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, pwani ya kaskazini na baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki kama ilivyotabiriwa. Aidha, ongezeko la mvua linatarajiwa katika miezi ya Novemba na Disemba, 2023. Vilevile, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari na Februari, 2024.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!