Home Kitaifa TMA YAONGEZA WIGO WA UTOAJI TAARIFA KUSAIDIA WAKULIMA KATIKA UZALISHAJI

TMA YAONGEZA WIGO WA UTOAJI TAARIFA KUSAIDIA WAKULIMA KATIKA UZALISHAJI

Na Magrethy Katengu

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema imeendelea kuongeza wigo wa utoaji taarifa za hali ya hewa kwa maeneo madogo madogo, ambapo msimu wa Vuli 2022 utaambatana na tabiri za wilaya zote themanini na sita zilizo kwenye kanda za nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya kaskazini na ukanda wa ziwa Victoria.

Hayo ameyasema Mwenyekiti wa Bodi ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi wakati akifungua rasmi Mkutano wa Wadau wa Utabiri wa Mvua za Vuli 2022 katika Ukumbi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam Agosti Mwaka huu

Utabiri huu wa msimu wa Vuli utaambatana na tabiri za wilaya zote themanini na sita (86) zilizopo kanda nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya kaskazini na ukanda wa Ziwa Viktoria. Hivyo mimi binafsi napenda kutoa pongezi nyingi sana kwa hatua hii kubwa ya kuongeza wigo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa hususani kwa watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wa sekta kaika maeneo mbalimbali ambao wamekuwa na uhitaji wa taarifa hizi kwenye maeneo yao” amesema Nyenzi

Aidha, Dkt Nyenzi amesisitiza ushirikiano kuhakikisha kwamba taarifa hizo zinawafikia watumiaji wa mwisho kwenye sekta mbalimbali ili kuweza kuchangia katika ukuaji wa uchumi na kuleta tija pamoja na kufuatilia kwa karibu, kuelewa, kupanga na kukabiliana na hali ya hewa inayotarajiwa katika sekta zao.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la hali ya Hewa Duniani, Dkt. Agnes Kijazi alieleza kuwa kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Matumizi Sahihi ya Taarifa za Hali ya Hewa kwa Maendeleo Endelevu” hivyo Ili kuendana na kaulimbiu hiyo, TMA imeendelea kuboresha taarifa zake kwa kutoa utabiri mahususi kwa sekta mbalimbali mwa kuongeza thamani taarifa zake za utabiri wa msimu na kujumuisha taarifa za maeneo madogo madogo kwa ngazi ya wilaya.

Wakati Serikali ya awamu ya sita ikiendelea na jitihada za kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo huduma za hali ya hewa, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kuweka msisitizo wa matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa kila sekta ili kuongeza tija katika uzalishaji” amesema Dkt. Kijazi.

Kwa upande wa mdau kutoka Wizara ya Kilimo, akizungumzia utabiri wa msimu uliopita Bw. Juma Makandi amesema mara baada ya kupata taarifa za utabiri wa msimu wa mvua za Masika za awali na zilizohuishwa, wizara iliaandaa tafsiri ya utabiri huo katika uzalishaji wa mazao ya chakula na kuwasilisha kwa wadau mbalimbali kwa utekelezaji wake.

Katika Mkutano huo, wadau walipata fursa ya kuona rasimu ya utabiri wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2022 na kuweza kutoa ushauri utaowezesha kuandaa mbinu na mipango ya kukabiliana na athari (hasi au chanya) za utabiri huo. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajia kutoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za VULI 2022 kupitia vyombo vya habari, tarehe 1 Septemba 2022.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!