Home Kitaifa TIGO YAENDELEA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUWEZESHA USAJILI NA UTOAJI WA VYETI VYA...

TIGO YAENDELEA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUWEZESHA USAJILI NA UTOAJI WA VYETI VYA KUZALIWA KWA WATOTO ZAIDI YA MILIONI 8 NCHINI

Na Adery Masta.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa Watoto zaidi ya milioni 8.8 wamesajiliwa  na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara kupitia Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri chini ya miaka mitano.

Mhe. Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango leo Desemba 08, 2023 katika viwanja vya Mbagala Zakhiem Jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi huu unahitimisha Mikoa 26 ya Tanzania bara ambapo Mkoa wa Dar es Salaam unatarajiwa kusajili jumla ya watoto 248,298 na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa bila ya malipo kupitia vituo 505 vya usajili ambavyo ni Vituo vya Afya na Ofisi za Watendaji wa Kata.

Akizungumza na waandishi wa Habari Meneja Mahusiano ya Nje Tigo Bi. Rukia Mtingwa amesema

“Tigo inayo furaha kwa mara nyingine tena kuendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) na Ubalozi wa Canada nchini Tanzania na wadau wengine wa maendeleo kwa kutekeleza mkakati huo wa usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano kwa mikoa 26 sasa Tanzania nzima

Kampuni ya Tigo imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini Tanzania. Tunajivunia mafanikio ya sekta hii.

Sote tunatambua umuhimu wa utambulisho na takwimu katika kuwezesha upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile afya, elimu na kadhalika. Hata katika usajili wa laini za simu tunahitaji kitambulisho halali ambacho chanzo chake ni cheti cha kuzaliwa. Kwa hiyo, umuhimu wa watoto wetu kusajiliwa na kupata vyeti wanapozaliwa ni jambo linalohitaji kupewa kipaumbele cha juu na wadau wote, Tigo imeendelea kuwekeza katika mradi wa usajili wa watoto tangu 2013 

Tigo inatambua ukweli kwamba cheti cha kuzaliwa ni kitambulisho cha awali cha mtoto kinachomwezesha kutambua uwepo wake na pia ni haki yake ya msingi. Hivyo basi, tunawahimiza wazazi na walezi kuchangamkia fursa hii na kuhakikisha watoto wote wamesajiliwa na kupewa vyeti.

Kwa mara nyingine tena tunapenda kuwashukuru wadau wote kwa kuendelea kushirikiana nasi, na nichukue fursa hii kuendelea kuihakikishia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wote wa maendeleo kuwa tutaendelea kushiriki katika miradi mbalimbali ya uzalishaji mali na inayolenga hasa katika kuendeleza matumizi ya TEHAMA kwa ustawi wa jamii na uchumi kwa ujumla”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!