Serikali kupitia kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) yapokea ujumbe wa wafanyabiashara kutoka nchi ya falme za kiarabu ya Oman ambao wamekuja nchini kuangalia maeneo mawili mahsusi ya uwekezaji katika kilimo na Mifugo.
Hayo yamesemwa leo tarehe 19 Julai, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) jijini Dar es salaam na Naibu Waziri wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) mara baada ya kupokea ujumbe kutoka nchi ya Oman.
Mhe. Kigahe amesema kuwa ujumbe huu kutoka Oman ni mafanikio ya ziara ya kikazi iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipotembelea nchi ya falme za kiarabu ya Oman mwezi June, 2022 ambapo Tanzania na Oman zilikubaliana kuendelea kushirikiana katika uwekezaji kwa manufaa ya Wananchi wa Tanzania na Oman.
Mhe. Kigahe amesema kuwa hadi kufikia mwezi June, 2022 Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) walikuwa wamesajili miradi 62 kutoka nchi ya Oman yenye thamani ya dola zaidi ya milioni 308.35 ambayo ilitarajiwa kutengeneza ajira zipatazo 2,488.
Mhe. Kigahe ameushukuru ujumbe wa Oman ulioongozwa na Mwenyekiti wa Makampuni kutoka Oman Bw. Saleh Alshanfari na kuwakaribisha kuwekeza nchini Tanzania kwani nchi yetu imeboresha kwa kiasi kikubwa mazingira ya biashara nchini kupitia mpango wa maboresho ya ufanyaji biashara BLUEPRINT uliopelekea kupungua kwa tozo 232, marekebisho ya sheria na uanzishwaji wa dirisha moja la huduma linalozikutanisha taasisi mbalimbali zikiwemo (TMDA, TBS, BRELA, Uhamiaji, Idara ya Kazi, GePG na OSHA).
Mhe. Kigahe amesema kuwa ni wakati sasa kwa sekta binafsi kutumia fursa ya uwekezaji nchini hasa soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Mkataba wa eneo huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ambao unatoa fursa ya kuwa na soko la pamoja la bidhaa na huduma lenye jumla ya nchi 55 zenye takriban watu Bilioni 1.2 na pato ghafi la taifa lenye jumla ya Dola za Kimarekani trilioni 3.4 na fursa za uchumi unaokua kwa kasi.
Balozi wa Tanzania nchini Oman Mhe. Abdallah Kilima amesema kuwa ujumbe uliofika nchini ni Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya uwekezaji na uendelezaji kilimo, Mtendaji Mkuu wa benki ya BADEA ambao ni wawezeshaji wa kifedha katika miradi hiyo, Kampuni ya Albashiry Meet Company na Oman food investment company limited.
Balozi Mhe. Kilima ameongeza kuwa madhumuni makubwa ya ziara hii ni kuja kuwekeza katika miradi ya kilimo na mifugo, nchi yao ni jangwa sisi tuna ardhi hivyo wamekuja kufanya uwekezaji mkubwa kwa ajili ya kuilisha Arabuni kupitia Oman.
“Makubaliano yaliyoingiwa na kampuni ya NARCO kwa mradi wa majaribio unatarajiwa kuanza ndani ya siku 45 ambapo Tanzania itapeleka nchini Oman ng’ombe hai 4,000 baadaye wataongezeka hadi kufikia ng’ombe 60,000 kwa mwaka hivyo wakulima na wafugaji nchini watafaidika na thamani ya mifugo yao kupitia mradi huu’’ Amesema Balozi Mhe. Kilima.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Revocatus Rasheli Amesema kuwa kituo kimepokea wawekezaji kutoka Oman na wa kutoka nchi za kiarabu ili kutekeleza makubaliano ya uwekezaji yaliyosainiwa.
Bw. Rasheli amesema kazi kubwa inayofanywa na kituo cha uwekezaji ni kuratibu makubaliano ya uwekezaji yaliyosainiwa na kuwapeleka kuwaonesha maeneo mbalimbali ya uwekezaji kwa kuwaunganisha na wawekezaji wa ndani na sekta binafsi kuwaeleza fursa za uwekezaji zilizopo na taratibu zinazotakiwa kufuatwa katika kuwekeza nchini.