Na WAF – MWANZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Saidi Mtanda amewataka watoa huduma za afya kwa njia ya tiba asili nchini kushirikiana na Serikali kukemea na kutokomeza vitendo vya ukatili ndani ya jamii.
Mtanda ametoa kauli hiyo Agosti 28, 2024 wakati akifungua juma la tiba asili na maadhimisho ya tiba asili kwa Mwafrika yanayofanyika kwenye viwanja vya Furahisha Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza.
“Waganga wa tiba asili mna mchango mkubwa katika kuimarisha afya za watanzania, hivyo tukiunganisha matumizi ya dawa zenu na zile za hospitalini wananchi watastawi kwa kuwa na afya njema”. Amesema Mhe. Mtanda na kuongeza.
“Ni rai yangu wote tuungane kutokomeza vitendo vya ukatili wa mauaji ya Albino na watoto ambayo yamekuwa yakiripotiwa hivi karibuni”. Amesisitiza Mtanda.
Aidha, Mtanda ametumia fursa hiyo kuwataka waganga wa tiba asili nchini kujisajili kwenye baraza la tiba asili na mbadala na kuhuisha leseni zao kila mwaka ili kuepuka kukumbwa na mkono sheria.
“Mimi ninaamini tiba hizi za asili zinapoboreshwa zinafanya kazi sawa na tiba hizi za kawaida na ndio maana Watanzania zaidi ya asilimia 60 wanatumia tiba hizi na zinawasaidia, wote tunatambua kwamba tiba asili na tiba mbadala zimekuwa na mchango mkubwa kwa wananchi na ofisi ya mkuu wa mkoa kupitia sekta ya afya”. Amesema Mkuu wa Mkoa huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti msaidizi baraza la tiba asili na mbadala nchini Dkt. Elizabeth Lema amesema waganga wa tiba hizo wametoka kwenye mfumo wa kufanya kazi zao kienyeji na sasa wanafanya kisasa na wakati mwingine wanatoa huduma jumuishi na wataalamu kutoka hospitali za kawaida ambao wanakiri kwamba tiba za asili zinamsaada mkubwa katika kutibu magonjwa mbalimbali.
Naye Msajili wa baraza la tiba asili na mbadala Martin Mgogwa amebainisha kuwa baraza hilo pamoja na kuwasajili linasimamia, kuthibiti na kuendeleza tiba asili nchini kwa kuhakikisha kila anayetoa huduma za tiba asili anasajiliwa pamoja na kuhuisha leseni kila mwaka katika eneo lake.