Home Kitaifa TIB YAWEKEZA BILIONI 980. 7 KATIKA MIRADI MBALIMBALI

TIB YAWEKEZA BILIONI 980. 7 KATIKA MIRADI MBALIMBALI

Na Magrethy Katengu

BENKI ya Maendeleo (TIB) imesema hadi kufikia Septemba 30, 2023 imewekeza jumla ya shilingi bilioni 980.7 kwenye Miradi mbalimbali ikiwemo ya Kilimo, Elimu,Nishati,Maji.

Akizungumza Oktoba 16, 2023 na Kaimu Mkurugenzi wa TIB Lilian Mbassy katika semina wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Benki hiyo katika kati ya Wahariri na Waandishi wa Habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Asilimia 93 ni Miradi ya kwenye Sekta Binafsi, asilimia ni Miradi ya Umma na katika Miradi hii asilimia 80 ni Miradi ya muda mrefu ya zaidi ya miaka mitano (5),” amesema Mbassy.

Akizungumza amebainisha miongoni mwa Miradi ambayo wamewekeza ni pamoja na Kilimo/Usindikaji, Madini na Uchakataji, Nishati na Maji na Utalii.

Mbassy akielezea matokeo ya uwekezaji huo, amesema katika Sekta ya Kilimo/ Usindikaji wa mazao ya Kilimo jumla ya Miradi 253 imekopeshwa.

Hata hivyo kwenye Sekta hiyo mikoa 23 na Wilaya 76 zimenufaika na uwekezaji huo ambapo jumla ya shilingi bilioni 334.7 ndiyo iliyowekezwa kwenye Sekta hiyo ya kilimo.

Kwamba kutokana na uwekezaji huo kwenye Sekta ya Kilimo zaidi ya wananchi 10,230 wamepata ajira huku Taasisi za kifedha 12, SACCOS 78 na Kampuni 128 zikiwa zimekodishwa.

Kwa upande wa Sekta ya Maji, Mbassy amesema jumla ya Miradi ya Maji 66 imekopeshwa ambayo ni Mamlaka za Maji sita (6) na Jumuiya za Watumia Maji Vijijini 60.

Ametaja mikoa iliyonufaika na Miradi ya Sekta ya Maji kuwa ni Dodoma, Singida, Shinyanga, Tanga, Mtwara, Iringa, Ruvuma na Morogoro.

Kwamba mpango ni kukamilisha Jumuiya za Watumia Maji Vijijini 100 ambapo hadi sasa wamekamilisha Jumuiya za Watumia Maji Vijijini 60.

Mbassy amebainisha kuwa wamefanikiwa kukamilisha kilometa 157 za mtandao wa usambaziji wa maji, ambapo jumla ya wananchi 750,000 wamenufaika na Miradi hiyo ya Maji.

Kwamba jumla ya shilingi bilioni 14.9 imewekezwa katika Sekta hiyo ya Maji na Usafi wa Mazingira, hivyo ameeleza kuwa kauli ya kumtua mama ndoo kichwani wanaitekeleza kwa vitendo.

Kuhusu Sekta ya Nishati, Mbassy amebainisha kuwa jumla ya Miradi sita (6) imenufaika na uwekezaji huo, kwamba mikoa iliyonufaika ni Dar es Salaam, Iringa, Ruvuma, Pwani na Manyara ambapo jumla ya shilingi bilioni 12.03 imewekezwa kwenye Sekta hiyo.

Amesema wamefanikisha kuzalishwa kwa megawati 8.84 ambazo zimeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa ambapo ameeleza kuwa Kaya 500,000 zimenufaika na Mradi wa UNIDO wa matumizi ya ethano kama chanzo mbadala cha Nishati safi ya kupikia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!