
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt, Suleimani Jafo (Mb) ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) kuhakikisha inatengeneza misingi sahihi ya upatikanaji fedha ili kutimiza malengo ya Taasisi hiyo katika kukuza wa uchumi wa viwanda.
Dkt. Jafo ameyasema hayo Machi 03, 2025 wakati wa uzinduzi Bodi ya Wakurugenzi wa TEMDO uliofanyika katika Taasisi hiyo jijini, Arusha.

Aidha amesema Wizara yake itashirikiana na Wizara ya Afya na TAMISEMI ili kuhakikisha taasisi za umma zinanunua vifaa tiba vinvyotengenezwa na TEMDO ili kuokoa fedha nyingi inayotumika kuagiza vifaa hivyo nje ya nchi.
Vilevile ameishauri Bosi hiyo kushirikiana na taasisi nyingine kama vile Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) na nyinginezo ili kupata fedha za kuendeleza miradi mbalimbali itakayoanzishwa katika Taasisi hizo.
Katika Hatua nyingine amewasihi Wajumbe hao wa Bodi pamoja na Watumishi wa TEMDO kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, ubunifu na upendo ili kuleta tija na ufanisi katika utendaji kazi na utoaji huduma kwa ummakutimiza malengo ya Taasisi hiyo katika kuleta taswira nzuri ya kuhakikisha maendeleo ya TEMDO yanakuwa.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Hashil Abdallah ameisisitiza Bodi hiyo kuhakikisha maendeleo ya viwanda yanakua ikiwemo utekelezaji wa Sera sanjari na kubuni miradi mbalimbali

Wakati huo huo,Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Temdo, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia ameahidi kuwa Bodi hiyo itafanya kazi kwa bidii katika kukuza maendeleo ikiwemo kubuni miradi yenye kuleta mapinduzi katika sekta ya viwanda.

Awali Mkurugenzi wa TEMDO, Prof Frederick Kahimba amesema , TEMDO imetengeneza na kusambaza vifaa tiba 2,262 vya aina mbali mbali ikiwemo vitanda, kabati za wodini, standi ya drip, vitanda vya mama wajawazito, vitanda vya uchunguzi, jokofu za kuhifadhia maiti na vichomea taka hatarishi.