Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema mchezaji wa timu ya Walemavu ya Tanzania ya Tembo Warriors Alfan Athuman Kiyanga aliibuka mfungaji bora kwa kuweka kapuni magoli 6 na kutunukiwa tuzo ya ufungaji bora, kwenye michezo mitatu ya kimataifa ya majaribio nchini Poland ambayo ilijumuisha pia nchi za Morocco, Italia, Uingereza na Poland.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo Bungeni Jana Juni 16, 2022 akiwa anatoa taarifa ya pongezi kufuatia maagizo ya Mhe, Spika Dkt. Tulia Akson aliyoitaka Wizara kuileta timu hiyo bungeni ili kuipa heshima ya mashujaa wa taifa hivi karibuni baada ya kufuzu kuingia kwenye mashindano ya dunia ya soka kwa walemavu hivyo kuandika historia kuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia kwenye mashindano hayo ambayo yatafanyika nchini Uturuki Oktoba mwaka huu.
Amefafanua kuwa ushindi huo ni mikakati madhubuti ambapo amesisitiza kuwa ilikuwa ni wakati wa Jasho na Damu, kufa ama kupona kwa ajili ya kupambania maslahi ya Taifa ambapo Tembo iliikongota’ Timu ya Morroco mabao 2 – 1,ikaipiku timu ya Sierra Leone bao 1 – 0, na iliichakaza timu ya Cameroon kwa mabao 5 – 0.
“Mheshimiwa Spika, baada ya kuwapa heshima hapa Bungeni mashujaa wetu Timu ya Taifa ya Soka ya Vijana ya Wanawake wenye umri chini ya Miaka 17 (Serengeti Girls), kwa mara nyingine tena leo hii nimesimama hapa mbele naomba idhini yako ya kuwatambulisha mashujaa wetu wengine hawa Timu ya Taifa ya Soka la walemavu (TEMBO WORRIORS) ambayo imealikwa hapa Bungeni na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo mahususi kwa ajili ya kupongezwa pamoja na kusalimiana ana kwa ana na Waheshimiwa Wabunge na Viongozi mbalimbali wa Serikali kwa ujumla”. Amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Ameongeza kuwa sambamba na mchezaji Kiyanga kuwa mchezaji bora kwenye mashindano hayo pia timu ya Tembo Worriors imepewa tuzo ya kuwa timu bora na yenye nidhamu katika michuano hiyo.
Aidha, amesema Serikali ndio iliyofanikisha safari hiyo kwa ajili ya kushiriki mechi hizo maalum za maandalizi ya Kombe la Dunia kwa watu wenye ulemavu.
“Nimatumaini yangu kuwa mazoezi hayo walioyapata yatawasaidia kujirekebisha na kujiimarisha zaidi kwani watakuwa wameona taswira ya mashindano ya kombe la Dunia” ameongeza Waziri Mchengerwa.
Kwa upande mwingine, Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa juhudi za ushindi huo wa timu hiyo kufuzu kombe la dunia zilichagizwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipomtuma Mhe. Kasim M. Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda kambini kuwaongezea Ari na hamasa wachezaji pamoja na kutoa kiasi cha Shilingi milioni 150 zilizosaidia kuitunza timu yetu ya Taifa pamoja na maandalizi mengine.
Ameongeza kuwa kwa sasa kambi ya timu hiyo inahamia Karatu mahali penye utulivu zaidi na ukimya ili wamalizie maandalizi yao kabla ya kwenda nchini Uturuki.
Kwa upande wake Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Akson ameipongeza timu hiyo kwa kupambana vilivyo na kuipeperusha vyema taifa ndani na nje ya nchi.
Katika ziara hiyo ya Tembo Worriors Bungeni Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Hassan Abbasi pamoja na Viongozi wengine walishiriki.