Watumishi wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) wametakiwa kutumia elimu waliyoipata na fursa ya ajira ya Serikali kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya Serikali na Taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa leo na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende wakati akifunga mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha mkoani Pwani kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi wapya kuhusu masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma.
Dkt. Luhende amesema kuwa ni muhimu kwa kila mtumishi kuendelea kujikumbusha masuala yote waliyofundishwa katika mafunzo hayo watakapokuwa katika vituo vyao vya kazi kwa kuwa mafunzo ndio dira kwa watumishi wote wa Serikali hasa watumishi wapya.
Amesisitiza kuwa ili utumishi wao uweze kuwa na tija, ufanisi na kuheshimika kwa Ofisi na Taifa kwa ujumla, kila mtumishi anapaswa kufanya kazi kwa kufuata Kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma kwa kuwa na tabia na mienendo inayozingatia utoaji wa huduma bora, utii kwa Serikali, utoaji wa huduma bila upendeleo, kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa umma, kuheshimu Sheria za nchi na kuepuka vitendo vyote visivyofaa ikiwemo kushawishi na kupokea rushwa.
Ameongeza kuwa OWMS inatarajia kuwa baada ya mafunzo hayo watumishi hao wataweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo hivyo kuiwezesha Serikali kunufaika na matokeo chanya yatakayopatikana na kuwa chachu katika kuratibu, kusimamia na kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake ndani na nje ya nchi.
Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sarah Mwaipopo amewashukuru watumishi hao kwa umakini walioonesha katika kufuatilia mafunzo hayo ambapo amewataka kuzingatia mambo yote waliyofundishwa katika mafunzo hayo ili kufikia malengo yaliyowekwa na OWMS katika uendeshaji wa mashauri.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo yameendaliwa kwa lengo la kuwapatia nyenzo watumishi hao kwa lengo la kuwanoa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa wakati huku akisisitiza kuwa mafunzo hayo yatakuwa endelevu kwa watumishi wote watakaojiunga na Ofisi hii.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wenzake Bi. Kumbukeni Mwinyimadi, Wakili wa Serikali ameishukuru OWMS kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu huku akiongeza kuwa mafunzo hayo yatawaongezea morali katika kutekeleza majukumu yao kwa bidii ikiwa ni pamoja na kuzingatia utawala wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.